
TABORA
Mkuu wa Mkoa wa Tabora,. Paul Matiko Chacha, amesema kuwa Serikali imeongeza juhudi katika mapambano dhidi ya dawa banda ili kuhakikisha afya za wananchi zinalindwa.
Mkuu wa Mkoa Chacha ameyasema hayo leo Julai 16, 2025 alipokuwa akifungua kikao Kazi cha Mamlaka ya Dawa, Vifaa Tba na Vitendanishi TMDA, na wahariri wa habar kilichofanyika mkoani Tabora kwa ajili ya kanda ya Magharibi ya TMDA ikijumuisha mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na TMDA katika kudhibiti Dawa hizo, na kwamba haitosita kuchukua hatua dhidi ya watu watakaojihusisha kusambaza na kuuza dawa bandia.


Wadau wa habari mna umuhimu mkubwa katika kushirikiana na Serikali kwenye mapambano haya, hivyo niwaombe kuendelea kushirikiana na TMDA kutumia kalamu zenu kutoa elimu kwa wananchi dhidi ya dawa bandia” amesema.
Aidha, amesema kumekuwepo na changamoto ya uwepo wa matangazo ya bidhaa za dawa za binadamu kiholela, na kuitaka TMDA kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali kudhibiti hali hiyo.
“Bidhaa hizi ni nyeti, zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa watumiaji endapo hazitazingatia viwango vya usalama, ubora na ufanisi, ndio maana TMDA wamekuwa wanahakikisha bidhaa hizi zinahakikiwa kabla ya kuingia sokoni, kwaajili ya kulinda afya ya watanzania na jamii kwa ujumla” amesema.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, maboresho makubwa yamefanyika katika sekta ya afya yakiwemo kuimarisha taasisi kama TMDA, kwa hiyo ni hatua muhimu kwa ustawi wa afya za watanzania.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, amesema mafunzo hayo kwa wahariri yanakusudia kusaidia kulinda afya ya jamii kwa kuelimisha kuhusu matumizi sahihi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi, sambamba na kuonya juu ya athari zitokanazo na matumizi ya bidhaa hafifu.
“Baada ya utafiti huu kukamilika, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kuchukua hatua stahiki kudhibiti tatizo hili,” alisema Dkt Fimbo mbele ya wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
Alieleza kuwa lengo la kikao hicho ni kuongeza uelewa wa wahariri kuhusu majukumu ya TMDA na kuonyesha mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.
Miongoni mwa mafanikio hayo, Dkt Fimbo alitaja usajili wa jumla ya dawa 8,332 katika kipindi hicho, hatua iliyosaidia kupanua upatikanaji wa dawa muhimu kwa wananchi na hivyo kuboresha huduma za afya nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikao hicho, Bi Joyce Shebe, alisema vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba.
“Uamuzi wa TMDA kutualika kwenye kikao hiki cha kazi ni hatua muhimu inayotupatia maarifa yatakayotuwezesha kuandika kwa ufanisi zaidi kuhusu masuala ya afya,” alisema.





