
Na: Hughes Dugilo, Tabora
Katika kuendelea kutimiza ndoto za makazi bora kwa Watanzania, Shirika la Nyumba la Taifa, (NHC), linatekeleza mradi mpya wa kisasa wa jengo la biashara na makazi mkoani Tabora uitwao Tabora Commercial Complex, unaojengwa katikati ya mji huo wa kihistoria.
Mradi huo ambao ni wa kwanza wa aina hiyo kujengwa mkoani Tabora, unatekelezwa kwa gharama ya Sh.Bilioni 4, ukitarajiwa kukamilika mwezi Aprili 2026, ukiwa jumuishi, ambapo tayari umeanza kuwanufaidisha wanachi wa kada mbalimbali kiuchumi, huku maombi ya nafasi za biashara na makazi yakifurika.
Hapana shaka mradi huo unaleta sura mpya ya mji wa Tabora, ulio na historia kubwa kisiasa, kiuchumi hata kiutamaduni na maendeleo ya Tanzania kwa ujumla.


Eminick Sanga ni Meneja wa NHC Mkoa wa Tabora, anaellza kuwa Mradi wa Tabora Commercial Complex ni mkubwa kama unavyoakisi na utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa mkoa huo, lakini pia kuna mwitikio mkubwa wa wateja walioomba nafasi katika jengo hilo.
Anasema “Hadi sasa NHC imeshapokea maombi zaidi ya 200 ya wateja wanaotaka kupangisha maeneo ya biashara, ofisi na makazi. Kwa kweli mradi ni mkubwa na mwitikio ni mkubwa. Tunamshukuru Mungu kupata mradi huu na mwitikio mkubwa pia” anaeleza Sanga.
Kwa mujibu wa Sanga jengo hilo linatarajiwa kuongeza chachu ya maendeleo mkoani Tabora, na kuongeza makusanyo ya kodi za serikali kutoka kwa NHC na watanzania watakaopanga kwenye jengo hilo na kufanya biashara zao.


“Tunashukuru sana kuwa na mradi huu mkubwa ni wa kimkakati, ambao utaleta maendeleo kwa wananchi wa Tabora”
Amebainisha kuwa mradi huo umeongeza kipato kwa wananchi wa Tabora kutokana na kupata ajira kwenye ujenzi, lakini pia umeongeza kipato kwa wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, kwani vifaa vingi vinavyotumika kununuliwa mkoani humo.
“Ni mradi ambao tayari umeanza kuleta manufaa. Wananchi wana ajira kwenye ujenzi, mama ntilie wana ajira kuuzia wafanyakazi chakula, lakini kubwa kuliko ni kwamba, mradi huu kabla haujakamilika, tayari tumeanza kuupangisha, kabla haujakamilika” anasema Meneja huyo wa NHC Tabora.


Akizungumzia mradi huo, Mkazi wa Tabora, Sebedia Jonas anaelezaa kwamba mradi huo ni wa kupigiwa mfano katika Mkoa wa Tabora na Tanzania kwa jumla kwani unaibadilisha Tabora na kuonekana ya kisasa.
“Rai yangu ni kwamba mradi huu utunzwe, na kama itafaa uweze kubadili mji wetu wa Tabora kuwa jiji kwa manufaa ya wananchi. Nalishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuiletea Tabora Mradi huu. “NHC ina macho mawili yalioona na kuamua kutuletea maendeleo haya” amesema Jonas.

Mhandisi wa Mradi huo wa Tabora Commercial Complex, Remigius Chrisostoms anaeleza kuwa jengo hilo ni la ghorofa nne utakaogharimu Sh Bilioni 4, unajumuisha maeneo ya maduka 50, una sehemu za migahawa na Benki kwa eneo la chini.
“Ghorofa ya kwanza eneo lote ni kwa ajili ya maofisi, kulingana na mahitaji ya wateja, lakini pia una sehemu za makazi ya watu zinazoendelea kuanzia ghorofa ya pili, ya tatu hadi ya nne” amesema Mhandisi Chrisostoms.
Kwa mujibu wa mhandisi huyo, ujenzi wa mradi huo ulianza mwezi Mei mwaka huu 2025, na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Aprili mwaka 2026.
“Mradi huu tumeuanza kwa kasi, tunamalizia hatua za mwisho za msingi, ili tuendelee na hatua nyingine kwa ufanisi. Jengo hili lipo katikati ya mji wa Tabora, na mwitikio wa wateja kutafuta nafasi za upangaji ni mkubwa, hii ni kutokana na upekee wa jengo hili, kwa kadiri wananchi walivyolishuhudia katika picha” amesema Mhandisi Remigius.

Naye, Febronia Luzuya mkazi wa Tabora mjini, anaesema kuwa mradi huo ukikamilika, utawawezesha wageni hasa kutoka nje ya mkoa huo kupata eneo zuri la kufikia kutokana na ukweli kwamba katika mji huo hakuna jengo la kisasa kama linalojengwa na NHC.
Aidha, ameeleza kwamba si wageni pekee watakaofikia eneo hilo, bali pia jengo hilo litawavutia wawekezaji kuwekeza mkoani Tabora, hivyo kufungua fursa zaidi za kibiashara, ajira na uchumi kwa wakazi wa mkoa huo.
“Jengo hili likikamilika, naamini litakuwa mahali salama kwa wafanyabiashara kuwekeza mali zao kwa ajili ya biashara na huduma kwa wananchi, tunaishukuru NHC kwa sababu awali hapakuwa na jengo jumuishi kama hili” ameeleza Febronia.




