Home BUSINESS BOT YASHUSHA KIWANGO CHA RIBA KUTOKA ASIMILIA 6 HADI 5.75

BOT YASHUSHA KIWANGO CHA RIBA KUTOKA ASIMILIA 6 HADI 5.75

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na Lilian Ekonga,  Dar es Salaam

Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetangaza kushusha kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kwa asilimia 5.75 kutoka asilimia 6, kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2025. Hii inamaanisha kuwa kiwango hicho cha riba kitakuwa cha chini kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha ya BOT, ambaye pia ni Gavanna wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, alifafanua uamuzi huu leo katika taarifa aliyoitoa katika makao makuu madogo ya BOT, jijini Dar es Salaam, baada ya kikao cha kamati kilichofanyika Julai 2, 2025.

“Hatua hii ni sehemu ya mwelekeo wa kisera katika kudhibiti kiwango cha riba kinachotumika katika soko la fedha, ambapo mabenki na taasisi nyingine za kifedha hutegemea kuanzisha viwango vyao vya riba,” alisema Bw. Tutuba.

Uamuzi wa kushusha riba hii unadhihirisha mabadiliko makubwa katika sera ya kifedha ya nchi, hasa baada ya Benki Kuu kuanza kutekeleza mfumo wa kuhamasisha mwelekeo wa riba Januari 2024. Mfumo huu ulilenga kutoa mwelekeo wa riba kwa mabenki na taasisi nyingine za kifedha, badala ya kutumia mfumo wa awali wa ujazi wa fedha.

Lengo kuu la mabadiliko haya ni kuwezesha ukuaji wa uchumi huku kikilenga pia kupunguza mfumuko wa bei. Kwa kushusha kiwango cha riba, Benki Kuu ina matumaini kwamba itasaidia kuongeza ukwasi wa fedha katika uchumi wa nchi, hivyo kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wananchi na sekta binafsi, huku pia ikichochea shughuli za kiuchumi kwa ujumla.

Kwa sasa, wadau wa uchumi wanasubiri kuona ni vipi mabenki yataathiriwa na mabadiliko haya ya riba na kama yataweza kutekeleza mipango ya kufadhili miradi ya maendeleo na biashara ndogo ndogo, ambazo ndizo tegemeo kuu la uchumi wa Tanzania.

Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wanasema kwamba uamuzi huu wa Benki Kuu unakuja wakati muhimu ambapo uchumi wa Tanzania unahitaji msukumo wa kifedha ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokikumba, kama vile ongezeko la gharama za maisha na changamoto za kimataifa.

Kama ilivyo kwa sera yoyote ya kifedha, wananchi wanatakiwa kuwa na uangalifu kwa kushirikiana na mabenki na taasisi za fedha katika kupata mikopo yenye manufaa, huku wakizingatia viwango vya riba vinavyobadilika kutokana na hali ya uchumi.