
Mkoa wa Mwanza —
Taasisi ya Ladies of New Millennium, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mama Tunu Pinda, imeonesha mfano wa kuigwa kwa taasisi binafsi kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na umaskini kupitia ziara ya kutembelea na kuchangia miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Katika ziara hiyo ya kikazi iliyofanyika katika Wilaya ya Ilemela, wajumbe wa taasisi hiyo walishuhudia mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN), hususan katika sekta za elimu, ujasiriamali na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Wakiwa katika Shule ya Sekondari Igogwe, waliona maboresho ya miundombinu yaliyofadhiliwa na TASAF kupitia afua za kijamii. Pia walikutana na wanufaika wa mpango huo waliofanikiwa kuanzisha miradi midogo ya kiuchumi kupitia mafunzo na mitaji waliyopewa.
Kwa kutambua mchango wa nishati safi katika kuboresha afya na mazingira ya kaya masikini, taasisi hiyo ilitoa mitungi ya gesi kwa baadhi ya walengwa, ikiwa ni mchango wao katika kuchochea matumizi ya nishati mbadala badala ya kuni na mkaa.
Katika hatua nyingine, wajumbe wa Ladies of New Millennium walifanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya Mayuganya, na kupata taarifa kuhusu utekelezaji wa mpango huo na mchango wake katika maendeleo ya jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Mkurugenzi wa Mifumo, Tathmini na Mawasiliano Bw. Japhet Boaz alieleza kuwa zaidi ya kaya milioni moja zimenufaika na mpango huo kwa njia mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, lishe na ajira ya muda.
Taasisi hiyo ilitoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuendeleza mpango huo na kuimarisha usimamizi wake, huku ikiisifu TASAF kwa uwazi na ufanisi katika utekelezaji wa miradi yake.
Wajumbe waliotembelea miradi hiyo kutoka Taasisi ya Ladies of New Millennium Tunu Rehani Pinda, Asina Kawawa, Blandina Mususa, Suzana Charles Majua, Frida Rugemalira.
Ziara hiyo imekuwa mfano hai wa namna sekta binafsi zinavyoweza kushirikiana na Serikali katika kuboresha maisha ya Watanzania, hususan kaya zenye kipato duni, na hivyo kuchochea maendeleo jumuishi na endelevu ya jamii.






