_▪️Rais Ouattara asisitiza uongezaji thamani wa mazao_
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameshiriki ufunguzi wa Mkutano wa siku mbili wa Maafisa Watendaji Wakuu barani Afrika ulioanza leo Mei 12, 2025, katika ukumbi wa hoteli ya Sofitel jijini Abidjan, Ivory Coast.
Mheshimiwa Majaliwa amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo ambao umefunguliwa na Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara na kuwakutanisha Maafisa Watendaji Wakuu zaidi ya 3000, wawekezaji na Wakuu wa Nchi na Serikali.
Akizungumza na washiriki wa jukwaa hilo, Rais Ouattara amesema kuwa mkutano huo utawawezesha washiriki kujadili changamoto zinazolikabili bara la Afrika na kutoa majawabu ya changamoto hizo katika maeneo ya uchumi, fedha, mazingira na biashara.
Ameongeza kuwa ili bara la Afrika liweze kuendelea kuimarisha uchumi wake, viongozi wanapaswa kuendelea kuweka na kutekeleza mikakati ya kuongezea thamani mazao yanayozalishwa.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameshiriki Mjadala wa Marais ulioendeshwa na Mwandishi wa Kujitegemea wa CNN, Larry Madowo na kuwashirikisha Marais wa Afrika Kusini, Rwanda, Mauritania na Makamu wa Rais wa Ivory Coast.
Akichangia mjadala huo, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema suala la amani na usalama Mashariki mwa Congo (DRC) limepitia hatua kadhaa za mazungumzo na mashauriano hadi kufikia hatua ya majeshi kuanza kujiondoa kwenye eneo hilo.
Amesema mazungumzo ya Nairobi, Rwanda na Qatar yalifanyika na yamesaidia kujenga msingi imara wa hatua iliyofikiwa hivi sasa lakini zaidi ni kutokana juhudi za wadau wengine wanaotaka amani wakiwemo viongozi wa dini.
“Kwenye masuala kama haya ni lazima tutambue kuwa matatizo ya Afrika yatapata suluhu za Kiafrika na hili ni bara letu kwa hiyo tunao wajibu wa kushughulikia matatizo yetu na siyo kutafuta ufumbuzi kutoka nje,” alisema na kushangiliwa.
Akichangia swali ni kwa jinsi gani bara la Afrika linaweza kujisimamia kiuchumi kwa kutumia rasilimali zake, Rais Paul Kagame wa Rwanda alisema kuna umuhimu wa sekta binafsi kuwezeshwa ili iweze kuchangia ukuaji wa uchumi barani humo.
“Hatuwezi kuhimiza sekta binafsi ishiriki kwenye ukuzaji wa uchumi kama Serikali zetu hazitawawezesha kwa kuwapa vivutio ikiwemo sera, sheria, kanuni pamoja na utawala bora. Nazungumza hivyo kwa sababu kuna mambo huwa tunakubaliana kwenye vikao lakini utekelezaji wake unachukua muda mrefu sana, na hii inakarahisha,” alisema.
“Hatuwezi kuacha hali hii iendele kwa sababu nguvu tunayo, maono tunayo, rasilmali tunazo na tunazo njia wa kutekeleza hayo,” alisema.
Naye Rais wa Mauritania, Mohamed Cheikh El-Ghazouani alisema maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanaweza kukua kupitia ushirikiano baina ya sekta binafsi na umma wwnye nia ya kujiletea maendeleo.
Baadaye leo jioni, Waziri Mkuu atashiriki mjadala ukaojumuisha mawaziri wakuu wanne kutoka Tanzania, Ivory Coast, Guinea na Cameroun.