Home LOCAL WAUGUZI WATAKIWA KUWA WAADILIFU, WAGUNDUZI KATIKA KAZI

WAUGUZI WATAKIWA KUWA WAADILIFU, WAGUNDUZI KATIKA KAZI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na, WAF-Iringa.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amewataka wauguzi kote nchini kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uzalendo, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda miiko na maadili ya taaluma ya uuguzi ili kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza leo Mei 12, 2025 katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Iringa, Dkt. Mollel amewaasa wauguzi kuendelea kuwa na nidhamu ya kazi, kuheshimu wateja wao, na kuhakikisha wanatoa huduma kwa huruma na ufanisi bila kujali changamoto zilizopo katika mazingira yao ya kazi.

“Wito wangu kwa wauguzi wote ni kuwa waadilifu, waendelee kutunza maadili ya taaluma yao. Taaluma ya uuguzi inahitaji moyo wa kujitolea, lakini pia ni taaluma inayohitaji uaminifu na uadilifu wa hali ya juu kwa sababu mnashughulika moja kwa moja na maisha ya watu,” amesema Dkt. Mollel

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amewataka wauguzi kuwa wabunifu na wagunduzi katika kazi zao, akisisitiza kwamba ubunifu una nafasi kubwa katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya, hasa katika maeneo yenye upungufu wa vifaa na rasilimali watu.

“Natoa changamoto kwa wauguzi kuwa wabunifu. Dunia inabadilika kwa kasi, hivyo hata nyie mnatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutumia maarifa yenu kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta ya afya. Tunaweza kuwa na mifumo bora ya kutoa huduma kama tutakuwa wabunifu,” ameongeza Dkt. Mollel.

Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani hufanyika kila mwaka Mei 12 ili kutambua mchango mkubwa wa wauguzi katika sekta ya afya duniani kote.Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wauguzi kutoka mikoa mbalimbali nchini, ambapo pia zilitolewa zawadi kwa wauguzi waliotambuliwa kwa umahiri na ufanisi kazini.