Home SPORTS SIMBA SC YASHINDWA KUTWAA UBINGWA KOMBE LA CAF

SIMBA SC YASHINDWA KUTWAA UBINGWA KOMBE LA CAF

Ndoto  za Simba SC kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika hazikutimia leo baada ya kutoa sare ya kufungana bao 1-1 na Renaissance Sportive de Berkane ya Morocco katika mchezo wa marudiano wa Fainali Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Matokeo hayo yanamaanisha RSB Berkane wanatwaa taji la CAF Confederation Cup kwa ushindi wa jumla wa 3-1 kufuatia kushinda mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita Uwanja wa Manispaa ya Berkane mjini Berkane.

Katika mchezo wa leo Simba SC walitangulia kwa bao la Mzambia, Joshua Mutale Budo dakika ya 17 akimalizia pasi ya winga mwenzake, Mkongo Elie Mpanzu Kibisawala – kabla ya kiungo wa Kimataifa wa Mali, Soumaila Sidibe kuisawazishia RSB Berkane dakika ya 90’+3.

Refa Dahane Beida wa Mauritania alimtoa kwa kadi nyekundu kiungo Yusuph Ally Kagoma dakika ya 50 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
Mshambuliaji Mganda, Steven Dese Mukwala aliunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu wa kiungo Muivory Coast, Jean Charles Ahoua dakika ya 76 na kufunga – licha ya refa kukubali bao hilo, lakini akabatilisha maamuzi yake baada ya msaada wa Marudio ya Picha za Video (VAR) kufuatia kughasiwa na wachezaji wa RSB Berkane.

Hii inakuwa mara ya tatu kwa RSB Berkane kutwaa CAF Confederation Cup baada yam waka 2020 na 2022, mwaka ambao pia walitwaa taji la CAF Super Cup.

Kwa Simba SC imekuwa mara ya pili wanamalizia nyumbani Fainali za CAF na kushindwa kutwaa taji baada ya mwaka 1993 pia kufungwa 2-0 na Stella Adjame ya Ivory Coast Uwanja wa Taifa, sasa Uhuru Jijini Dar es Salaam kufuatia kutoa sare ya bila mabao awali Jijini Abidjan.