Home LOCAL PUMA ENERGY TANZANIA KUPITIA UPYA MPANGO MKAKATI WA BIASHARA

PUMA ENERGY TANZANIA KUPITIA UPYA MPANGO MKAKATI WA BIASHARA

Dar es Salaam, Mei 26, 2025 — Wawekezaji wa PUMA Energy Tanzania, ambao ni Serikali ya Tanzania na Puma Investments Limited, wamekubaliana kufanya mapitio ya mpango mkakati wa biashara wa kampuni hiyo ndani ya mwaka huu.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mpango huu mpya wa biashara unalenga kuongeza uwekezaji, kupanua mtandao wa usambazaji, na kuongeza idadi ya bidhaa, kwa lengo la kuimarisha mchango wa wa kampuni hiyo katika uchumi wa Tanzania, na kukuza maendeleo ya sekta ya nishati.

Hayo yalibainishwa Jumatatu, Mei 26, 2025 wakati wa ziara ya viongozi wa ngazi ya juu wa PUMA Energy kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina iliyopo jijini Dar es Salaam, wakiongozwa na Bw. Mark Russel, Afisa Mtendaji Mkuu wa PUMA Energy Duniani.

Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema mapitio ya mpango mkakati wa biashara yanalenga kuona ukuaji wa kampuni unalingana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa, pamoja na kufungua milango ya fursa mpya katika sekta ya nishati.

“Uongozi wa kampuni na bodi lazima waangalie upya mpango mkakati wa biashara ndani ya mwaka huu ili kuanzia mwaka ujao tuweze kuzitumia vizuri fursa tulizonazo,” alisema Bw. Mchechu, huku akiweka wazi kuwa utekelezaji wa mpango mkakati mpya utaanza Januari mwakani.

PUMA Energy Tanzania ni kampuni inayomilikiwa kwa asilimia 50 na Serikali ya Tanzania na asilimia 50 na Puma Investments Limited.

Kampuni hii ni tawi la Puma Energy Holdings Pte Ltd, sehemu ya Trafigura PE Holding Ltd.

Bw. Mchechu alisisitiza kuwa uwekezaji wa Serikali katika PUMA ni mkakati muhimu unaolenga kuiwezesha Serikali kuwa na ushawishi mkubwa katika sekta ya nishati na mtandao wa usambazaji wa mafuta nchini.

Kwa upande wake Bw.Russel, alisema Tanzania ina fursa nyingi za kukuza biashara, ikiwemo miradi ya gesi ya asilia (LNG) na gesi ya kupikia (LPG).

“Tuna mpango wa kupanua huduma na kuongeza aina za bidhaa tunazotoa kwa jamii. Kupitia ushirikiano wetu na Serikali, tutashirikiana kufungua fursa zaidi na kukuza biashara hii,” alisema Bw. Russel.

Bw. Ben Quattara, Mkuu wa kampuni za PUMA Energy Afrika, alibainisha kuwa Tanzania ni mshirika muhimu katika biashara za PUMA barani Afrika na kampuni ina nia ya kuendeleza uwekezaji na faida zaidi hapa nchini.

Bi. Fatma Abdallah, Mkurugenzi Mtendaji wa PUMA Energy Tanzania, aliripoti ongezeko la asilimia 51 la faida mwaka 2024 na kufungua vituo vipya vya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) pamoja na upanuzi wa biashara ya gesi ya kupikia (LPG) katika mikoa kadhaa ikiwemo Dodoma, Mwanza, na Arusha.

“Tegemeeni mambo makubwa kutoka PUMA Tanzania katika miezi na miaka ijayo,” alimalizia Bi. Abdallah