Home BUSINESS NHC YAIN’GARISHA MASASI

NHC YAIN’GARISHA MASASI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

-Jengo la Sh2.7 bilioni lazinduliwa

-Kukamilika Septemba 

-Wapangaji wameshajaa

Mwandishi Wetu

Mei 18,2025 ni siku ambayo NHC imeandika historia mpya kwa mji wa Masasi, wilayani Masasi mkoani Mtwara.

NHC imeandika historia hiyo kwa kuzinduliwa ujenzi wa jengo jipya, ambalo ni Kituo cha Biashara, Masasi Commercial Complex lililowekwa jiwe la msingi na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi.

Jengo hilo litakapokamilika litabeba na kuibadili sura ya Masasi na kuifanya mpya, ikizingatiwa kuwa lipo katika barabara kuu. 

Ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya msukumo ilionao Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuchochea mapinduzi ya sekta ya nyumba na makazi bora ya kisasa, lakini pia kuchagiza kasi ya ukuaji uchumi wa taifa kwani shirika hilo linatekeleza dira yake iliyojiwekea.

Katika mahojiano, Muungano Saguya, Meneja Uhusiano na Habari wa NHC, akiwa Masasi kwenye ghafla ya uwekaji Jiwe la Msingi la ujenzi wa Masasi Commercia Complex anazungumzia mradi huo na mingine inayotekelezwa na shirika hilo.

“Nashukuru leo tumepata fursa, Mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la Msingi katika jengo hili Masasi Commercial Complex. Ni jengo la kisasa.”

Saguya anasema jengo hilo linafungua fursa mpya kwa watanzania, wafanyabiashara wa kada mbalimbali kuwekeza na kufanya shughuli zao katika jengo jipya la kisasa.

“Kama mlivyosikia…; jengo hili litagharimu Shilingi bilioni 2.7.Tunatarajia litakamilika ifikapo Septemba mwaka huu 2025. Anasema kwenye miji yote ambayo inakua kwa kasi kubwa, NHC imejenga majengo makubwa. “Kahama tumeweka jengo kama hili, leo tupo Masasi. Tumeweza kuweka majengo haya kwa ajili ya kuruhusu watanzania kuwekeza biashara zao. Hii itaweza kusaidia Serikali kuweza kukusanya mapato makubwa kutokana na kodi kutoka kwa wafanyabiashara.”

Saguya anasema hilo pia litaiongezea Shirika la Nyumba la Taifa fedha nyingi zaidi, ambazo zitalisaidia shirika kujenga nyumba nyingine kwa ajili ya watanzania.

Anasema katika hotuba ya uzinduzi wa Masasi Commercial Complex, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Ismail Ali Ussi, ameiomba NHC iende maeneo mbalimbali nchini kuwekeza majengo kama lilivyo Masasi Commercial Complex na kwamba kauli ya kiongozi huyo ni maelekezo kwa shirika kwani anafanya kazi kwa niaba ya Serikali.

“Kujenga majengo kama haya, kujenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa Serikali, hiyo ipo  kwenye mipango ya NHC, kuhakikisha tunafika kila halmashauri ya mji na wilaya kuona fursa zilizopo. Tukikubaliana na halmashauri hizo, tutaweza kwenda kujenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa umma,” anasema Saguya.

Akizungumzia matarajio ya shirika hilo Meneja Uhusiano na Habari anasema NHC inatarajia kukuza uchumi kwenye  miji inayokua kwa kazi.

Anasema kabla ya kutekeleza mradi wowote wa ujenzi, shirika hilo hufanya utafiti ili kujua mahitaji katika miji husika.

“Tulifanya utafiti katika Mji wa Masasi na miji mingine hapa nchini na kujiridhisha kwamba tutapata wateja wa kutosha na kweli. Mpaka sasa jengo hili la Masasi Commercial Complex limeshajaa. Wateja wameshajiorodhesha wakihitaji kupangisha na hakuta tena nafasi,” anasema Saguya.

Anasema NHC ina uhakika baada ya jengo hilo kukamilika wateja watajaa kwa asilimia 100, hivyo kuweza kuanza kurejesha fedha zilizotumika kwa ujenzi lakini pia kuliwezesha  shirika kujenga majengo mengine kwa ajili  ya watanzania maeneo mbalimbali nchini.

Saguya anasema ujenzi wa nyumba unaofanywa na NHC ni endelevu na unafanywa kwa kuzingatia mahitaji ya watanzania.

“Tuna kitengo ndani ya shirika huwa kinafanya utafiti na kuishauri menejmenti ya shirika kwamba eneo fulani lina mahitaji makubwa ya nyumba;

Kwa kweli tuna mahitaji makubwa za makazi na ndio maana NHC imeanza kubadili miji yetu kwa kushirikiana na  sekta binafsi, kwa kubomoa majengo makuukuu katikati ya miji ili kujenga majengo ya ghorofa.

“Hayo yatatoa nafasi kubwa zaidi kwa wananchi kupata maeneo ya kufanyia biashara na maeneo ya kuishi. Mfano eneo la Kariakoo, tumeshabomoa majengo 21, miradi ikikamilika kujengwa thamani yake ni zaidi ya Shilingi bilioni 271, kabla ya kujengwa upya ilikuwa na thamani ya chini karibu Shilingi bilioni 70,” anasema Saguya.

Anabainisha kwamba majngo hayo awali yalikuwa na wapangaji wasiozidi 172, lakini baada ya kubomolewa na kujengwa upya yatakuwa na wapangaji zaidi ya 2,150.

“Hapo unaweza kuona jinsi NHC inavyotumia mbinu mbalimbali kufanya utafiti na kushirikisha sekta binafsi kufahamu maeneo yenye masoko na kuwajengea watanzania kwa ajili ya makazi, masoko na matumizi mengine ya kijamii,” anasema Saguya.

Anabainisha kuwa katika Wilaya ya Masasi NHC imejenga jengo jingine maeneo ya Chilungutwa, ambalo ni ghala, likisaidia wakulima kuhifadhi mazao yao.

Anasema jengo hilo limejengwa baada ya kufanyika utafiti na kujiridhisha kuwepo kwa mahitaji.

Saguya anasema NHC ina sera ya uwekezaji, ambayo huliwezesha shirika kupima na kutoa mwongozo kwamba majengo mangapi yanaweza kujengwa na ya aina gani.

Kwa mujibu wa Saguya, kwa sasa NHC ina majengo na nyumba zaidi ya 3,000 inayomiliki yenye sehemu za nyumba zaidi ya 18,000 nchini zilizojengwa kwa miaka tofauti.

“Kwa mwaka huu wa fedha unaoendelea, NHC ina miradi zaidi ya 30 inayotekelezwa ikiwa katika hatua mbalimbali. Miradi hiyo ikikamilika itakuwa na maeneo mengi kwa ajili ya biashara na makazi, lakini Mpango Mkakati wa shirika wa miaka 11, unatuelekeza namna ya kufanya uwekezaji wenye tija kwa NHC na taifa. Uwekezaji huo ni endelevu na tunaendelea kuufanya kwa Kadiri tunavyoendelea kupata mahitaji hayo,” anahitimisha Saguya.   

Neno la Meneja wa Mradi

Akitoa historia ya ujenzi wa mradi wa kituo hicho mbele ya mgeni rasmi, meneja wa mradi huo, Gofrey Mkumbo kupitia risala aliyoisoma, ameeleza ulianza kutekelezwa Julai 25 mwaka 2024, baada ya NHC kukamilisha taratibu zote za ujenzi katika Halmashauri ya Mji wa Masasi.

“Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika, Septemba 14, mwaka 2025, ukiwa na maeneo mbalimbali ya biashara kama vile benki, ofisi, migahawa na maduka ya biashara mbalimbali,” amesema Mkumbo akiongeza:

“Ukamilifu wa ujenzi huu mpaka hapa ulipo ni asilimia 76. Hii ikijumuisha na taratibu zote za manunuzi ambazo zimeshakamilisha kwa vifaa vyote vya ujenzi ambavyo havijafika hapa kutokana na changamoto ya ubovu wa barabara za ukanda wa kusini.”

Hata hivyo, Mkumbo amesema vifaa hivyo vitaanza kuwasili ndani ya siku saba kuanzia Mei 18, 2025 hivyo kuendelea kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha biashara.  

Kuhusu lengo la mradi huo, Mkumbo ameyataja ni kuboresha huduma za kijamii na wafanyabiashara wa  ndani na na nje ya Masasi.  

Kwa niaba ya NHC, Mkumbo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayofanya kazi chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na mipango thabiti na kuinua uchumi wa taifa.

Akitoa maelezo kuhusu jengo hilo, Mshauri Elekezi wa mradi huo wa Kituo cha Biashara Masasi, Noel Mihanjo amesema kupitia mradi anaousimamia kuna faida mbalimbali kwa wananchi wa Masasi.

Amezitaja kuwa ni pamoja na kutoa ajira za muda kwa wananchi wakati na baada ya ujenzi, kukuza uchumi kwa wafanyabiashara na kuleta mwonekano mzuri kwa mji wa Masasi. 

“Pia kukuza uchumi wa wafanyabiashara wa eneo la Masasi, kuleta mwonekano mzuri wa Masasi hasa eneo hili, kandokando ya barabara kuu.”

Amebainisha kuwa hadi ulipofikia, mradi huo fedha ambazo zimeshatumika ni Shilingi 1,450,718,159.94.          


Akiweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Kituo cha Masasi Commercial Complex, Kiongozi wa Mwenge Kitaifa, Ismail Ali Ussi amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kwa kazi kubwa ya kutekeleza kwa vitendo ndoto za kuboresha huduma za jamii na wafanyabiashara nchini kupitia sekta ya nyumba.

Ussi amesema kwa kujenga majengo bora ya kisasa NHC inayochochea kasi ya maendeleo na uchumi wa taifa.

“NHC mnafanya kazi kubwa kwenye sekta ya ujenzi mkiisaidia Serikali kutimiza ndoto za kuboresha huduma ya makazi bora na maeneo bora ya biashara kwa jamii,” amesema Ussi.

 Jengo hilo la kisasa limejengwa Mtaa wa Madaraka katika Kata ya Jida, wilayani Masasi likiwa na maeneo mbalimbali ya kibiashara ikiwamo benki, maduka, migahawa na ofisi za kufanyia biashara mbalimbali.

Ussi anasema Serikali imekuwa na jitihada za makusudi kuwaletea wananchi wake maendeleo, jambo ambalo limeshuhudiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, kuweka jiwe la msingi la jengo hilo linalobadili sura ya maendeleo kwa wananchi wa Masasi.

“Leo hii tupo hapa na NHC baada ya wao kufanya utafiti na kubaini hapa Wilayani Masasi kuna uhitaji wa masuala ya fedha, benki na mahitaji mengine ya kijamii. Tunawashukuru NHC kwa kazi kubwa, wameutendea haki Mwenge wa Uhuru kwa sababu jengo hili litawakusanya wafanyabiashara wengi na wananchi wetu watapata huduma,hakuna  mwananchi atakayekosa huduma anayohitaji katika jengo hili,” amesema Ussi.

Amewaomba wananchi kuonyesha ushirikiano kwa NHC katika matumizi bora ya uwekezaji huo wa eneo la huduma za kijamii, akieleza pia NHC imeonyesha kwa vitendo jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuwaletea wanachi maendeleo wanayohitaji.

Mwisho.