Home BUSINESS NHC YAENDELEA KUJENGA NYUMBA BORA NA NAFUU KWA WATANZANIA

NHC YAENDELEA KUJENGA NYUMBA BORA NA NAFUU KWA WATANZANIA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Dodoma, Mei 29, 2025 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) inaendelea kutekeleza kwa vitendo dhamira ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata makazi bora, salama na yenye gharama nafuu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuondoa changamoto za makazi na kupanga miji kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, alieleza kuwa NHC linaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ujulikanao kama Samia Housing Scheme, ambao unalenga kuwawezesha Watanzania wengi kumiliki makazi yao.

“Tunaendelea kutafuta teknolojia mpya na bora kutoka mataifa mengine ili kupunguza gharama za ujenzi. Lengo ni kuhakikisha nyumba zinazojengwa na NHC zinauzwa kwa bei ambayo Mtanzania wa kawaida anaweza kumudu,” alisema Mhe. Ndejembi.

Katika hatua za kuboresha mazingira ya kumiliki nyumba, Waziri Ndejembi alisema Serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye nyumba zenye thamani ya chini ya shilingi milioni 50, na sasa inatazama uwezekano wa kuondoa VAT pia kwa nyumba zenye thamani ya hadi milioni 100 ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Aidha, alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya usimamizi wa ardhi kwa kuhimiza matumizi ya mfumo wa TEHAMA wa IARI-VI, huku ikipiga marufuku matumizi ya mfumo wa zamani wa MOLIS ambao ulichangia migogoro mingi ya ardhi ikiwemo utoaji wa hati mbili kwa kiwanja kimoja.

 “Kuanzia leo ni marufuku kuendelea kutumia mfumo wa zamani. Tunataka hadi mwaka 2027 mfumo wa IARI utumike nchi nzima,” alieleza.

Katika hoja nyingine, Waziri Ndejembi aligusia pia migogoro ya ardhi ikiwemo ule wa Wapare kwa Baba Askofu ambapo alieleza kuwa tayari fedha zimepatikana kwa ajili ya upimaji wa maeneo na kutatua mgogoro huo. Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kusikiliza pande zote katika migogoro mbalimbali ya ardhi ili kuhakikisha haki na amani vinapatikana kwa wananchi.

Pia, alieleza kuwa kuna nyumba zaidi ya laki mbili (200,000) katika maeneo yanayohitaji ufumbuzi wa migogoro, na Serikali kwa kushirikiana na wabunge na viongozi wa mitaa itaendelea kushughulikia changamoto hizo kwa ufanisi.

Katika kuchagiza kasi ya utendaji kwenye sekta ya ardhi na makazi, Waziri huyo alifichua kuwa Serikali kupitia maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetoa magari zaidi ya 50 kwa maafisa ardhi ili kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wananchi.

Akihitimisha, Waziri Ndejembi alisema kuwa ardhi ya Tanzania bado ni ile ile tuliyoachiwa tangu uhuru mwaka 1961 wakati taifa likiwa na watu milioni 9, lakini sasa nchi ina watu zaidi ya milioni 60, hivyo matumizi bora ya ardhi ni jambo la lazima.

 “Kama hatutajenga juu, tutaishia kutumia ardhi yote. Tunapaswa kulinda ardhi yetu kwa kupanga miji vizuri na kujenga nyumba za gharama nafuu,” alisisitiza.

Waziri pia aliahidi kufanyia kazi hoja zote za wabunge zilizowasilishwa kwa maandishi, na kusisitiza kuwa Serikali ipo makini kuhakikisha sekta ya ardhi inapata mageuzi kwa kuweka mifumo madhubuti ya kuondoa migogoro na kuleta maendeleo ya kweli.

Nao Wabunge waliotoa michango yao walitaka Shirika la Nyumba la Taifa kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba nafuu na kuiomba Serikali kuliwezesha Shirika kukamilisha jukumu hilo. Bajeti ya Wizara hiyo imepitishwa.