Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na Mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango wameshiriki Misa Takatifu ya Dominika ya Sita ya Pasaka katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro – Blockhauss Jijini Abidjan nchini Ivory Coast leo tarehe 25 Mei 2025. Misa hiyo imeongozwa na Padre Felicien Aguie.
Akiwasalimu waumini mara baada ya Misa hiyo, Makamu wa Rais amewapongeza waumini hao kwa kuendelea kumcha Mungu na kushiriki katika ibada hizo muhimu.
Makamu wa Rais amewapongeza wakina Mama wa kanisa hilo ambao wameadhimisha siku ya Mama Duniani kanisa hapo kwa malezi mema kwa watoto na kushiriki katika kudumisha amani.
Amewasihi wakina Mama wote kuendelea kusimama imara siku zote katika kuhamasisha amani ili kuweza kuwakuza watoto katika mazingira mema na yenye ustawi. Amesema siku zote ni muhimu kukumbuka kwamba Yesu Kristo aliacha duniani amani na sio vita.
Kwa upande wake Padre Felicien Aguie ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kudumisha amani na hatua mbalimbali ambazo imekuwa ikuchukua katika kutafuta amani Barani Afrika. Amesema Tanzania inatajwa kama nchi nzuri kutoka kwa watu mbalimbali wanaoitembelea nchi hiyo.
Katika Ibada hiyo ambayo imetumika kuiombea Tanzania, Makamu wa Rais ameongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ivory Coast mwenye Makazi yake nchini Nigeria Balozi Selestine Kakele.
Makamu wa Rais yupo nchini Ivory Coast kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mikutano ya Mwaka ya Bodi za Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) itakayofanyika kuanzia tarehe 26 hadi 30 Mei, 2025 Jijini Abidjan.