Home LOCAL MAKAMO WA RAIS DKT.MPANGO ASHIRIKI MAJADILIANO  NA VIONGOZI WA JUU KUHUSU UMUHIMU...

MAKAMO WA RAIS DKT.MPANGO ASHIRIKI MAJADILIANO  NA VIONGOZI WA JUU KUHUSU UMUHIMU WA KUTUMIA RASILIMALI ZA BARA LA AFRIKA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema maendeleo ya Tanzania katika uendelezaji miundombinu ni kutokana na ufanisi katika mapato ya kikodi, ushiriki wa sekta binafsi pamoja na uimarishaji wa masoko ya mitaji na dhamana inayotumika katika kufadhili miradi hiyo.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Makamu wa Rais amesema hayo wakati aliposhiriki majadiliano ya Viongozi wa Juu kuhusu “Umuhimu wa kutumia Rasilimali za Bara la Afrika kwa ufanisi ili kuchochea Maendeleo” yaliyofanyika wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika katika Hoteli ya Sofitel Ivoire Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.

Amesema kutokana na umuhimu wa miundombinu katika mageuzi ya kiuchumi nchini Tanzania, Serikali ilihitaji kufanya kazi zaidi katika kukusanya fedha ya uendelezaji wa miundombinu ikiwemo Reli ya kisasa (SGR) pamoja na barabara kuu ambazo zitaunganisha mataifa mbalimbali na kuwezesha ufanyaji biashara.

Makamu wa Rais ametaja juhudi za serikali katika ukusanyaji mapato ya ndani na kufadhili miradi ikiwemo kuimarisha usimamizi wa kodi kama vile ukusanyaji kupitia mifumo ya kielektoniki, kuwepo kwa Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko ya walipa kodi ili kuwawezesha walipa kodi kuweza kutoa changamoto zao pamoja na kukuza wigo wa soko la mitaji na dhamana kama vile uwepo wa hatifungani mbalimbali.

Hatua zingine ambazo Tanzania imepitia katika kuimarisha miundombinu ni pamoja na matumizi ya mifuko ya hifadhi ya jamii katika ujenzi wa barabara na madaraja pamoja na kutumia vema mikopo nafuu kutoka mashirika ya fedha kimataifa na nchi marafiki.

Makamu wa Rais ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na Rais wa AfDB anayemaliza muda wake Dkt. Akinumwi Adesina kwa kushirikiana vema na Tanzania katika kipindi cha uongozi wake ikiwemo kuwezesha ujenzi wa barabara, uwanja wa ndege pamoja na reli ya kisasa (SGR) kuelekea nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo.

Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya nishati kwa lengo la kuharakisha maendeleo ikiwemo uwekezaji mkubwa katika mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao umekamilika na unazalisha megawati 2115. Pia uwekezaji katika miradi mingine ikiwemo matumizi ya gesi asilia pamoja kuanza uzalishaji wa nishati ya joto ardhi ambayo itaanza kwa kuzalisha megawati 500.