Asema Serikali haitomvumia mtumishi atakayethibitika kuhusika na wizi_
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mwanza uhakikishe unakamilisha uchunguzi wa watumishi wa Hospitali ya wilaya ya Sengerema wanaodaiwa kuhusika na wizi wa vifaa hospitalini hapo ili watakaothibitika wachukuliwe hatua za kisheria.
”Watumishi mnatakiwa kuwahudumia wananchi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa na Serikali haitomvumilia yeyote atakayethibitika kuhusika na wizi. Ni muhimu sana kutunza vifaa, hapa tumeleta pikipiki tatu zimeibiwa, vifaa vya ujenzi na vifaa tiba vimeibiwa na matairi ya gari la wagonjwa yameibiwa mnataka litembee vipi.”
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Mei 19, 2025) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi Hospitali ya wilaya ya Sengerema akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza, ambapo amewasisitiza watumishi kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Amesema Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma mbalimbali zikiwemo za afya karibu na makazi yao ili kuwaondolea usumbufu na gharama za kufuata huduma hizo mbali na makazi yao, hivyo ni muhimu kutunza rasilimali hizo na watumishi wote watakaobainika kuhusika na wizi wachukuliwe hatua.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Dkt. Darison Andrew amesema mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo ulianza kutekelezwa mwaka 2020, ambapo umekuwa ukitekelezwa kwa awamu na tarehe 16 August, 2023 ilianza kutoa huduma huku ujenzi huo ukiendelea.
Amesema ujenzi huo hadi kukamilika unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.1, ambapo mbali na Serikali kutoa fedha za ujenzi pia ilitoa shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. “Pamoja na kupatiwa kiasi hicho cha fedha, hospitali yetu pia imepokea vifaa tiba mbalimbali toka Serikalini vyenye thamani ya shilingi milioni 418 ambavyo vinatumika kutolea huduma”.
Amesema mradi wa ujenzi unaotarajiwa kuendelea katika hospitali hiyo ni ujenzi wa jengo la huduma binafsi (private ward), ujenzi wa uzio kuzunguka hospitali, njia za watembea kwa miguu (Walkways), jengo la huduma ya mama na mtoto (RCH), jengo la huduma za chanjo (IVD) na nyumba 10 za watumishi..