
* Asema Afrika lazima iendelee kuimarisha mazingira wezeshi kwa kampuni bunifu za kidigitali
Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza wadau wa elimu barani Afrika kuendeleza mkakati na ushirikiano utakaowezesha mageuzi ya kidigitali katika sekta ya elimu.
Dkt. Biteko ametoa rai hiyo Mei 8, 2025 jijini Dar es salaam wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la 18 la eLearning Afrika.
“ Tanzania inaendelezo dhamira yake ya mageuzi ya kidigitali katika elimu na tungependa kushirikiana na Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wanazuoni ili kufanya e- learning kuwezeshwa kwa ghrama nafuu kwa wote ,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Tanzania imedhamiria kuongoza katika mageuzi ya kidigitali barani Afrika ambapo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inatambua kuwa mageuzi ya kidijitali ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kijamii na ushindani wa kimataifa. Ili kufanikisha hili, Tanzania imeandaa mifumo kadhaa ikwemo Sera ya Taifa ya TEHAMA na Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali Tanzania 2024-2034.
Dkt. Biteko amesema kuwa Mkakati wa Taifa wa Elimu ya Kidijitali na Programu ya Tanzania ya Kidijitali zinalenga kuimarisha miundombinu na huduma za kidijitali, kuhakikisha teknolojia muhimu, vifaa, muunganiko na rasilimali za e-learning vinafika maeneo mbalimbali nchini, aidha nchi zingine pia zitumie rasilimali zao katika kusaidia mageuzi ya kidijitali katika nchi zao.
Amewahimiza wadau wa kongamano hilo kuwa ili mageuzi ya kidijitali ya Afrika yaweze kufanikiwa, lazima kuwezeshwa kwa nguvu kazi yenye ujuzi kuanzia umri mdogo. Tanzania imefanya marekebisho ya Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo mwaka 2023 na kuwa ni mfano muhimu, ikisisitiza uendelezaji wa ujuzi kuanza elimu ya msingi.
“Sera hii pia inakuza matumizi ya teknolojia za kidijitali ili kukabiliana na upungufu wa walimu, kupanua upatikanaji wa elimu, na kuboresha ubora wa kujifunza. Mbinu hii inawaandaa wanafunzi kwa ajili ya baadaye na kuwawezesha waelimishaji kwa kuwapa zana bora za kufundishia katika nyakati za kidijitali,” amesema Dkt. Biteko.
Pamoja na hayo amesema kuwa Afrika lazima iendelee kuboresha mazingira kwa kampuni za kibunifu ya ndani kwa kuunda sera saidizi zinazokuza ubunifu na ujasiriamali ili kusaidia kukuza masoko ya ndani kwa teknolojia zinazoweza kuhamishwa na kuwezesha mataifa ya Afrika kuongeza ufanisi wa rasilimali, kupunguza ucheleweshaji na kuharakisha mageuzi ya kidijitali.
Pia amebainisha kuwa ni muhimu kwa Bara la Afrika kuwabakisha wataalamu wenye ujuzi ndani ya Afrika na kushirikisha diaspora ili kuchangia ukuaji wa bara hilo. Kwa kuifanya Afrika kuwa kitovu cha maendeleo ya kiteknolojia.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema Tanzania imeendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu kwa kuhamasisha matumizi ya akili mnemba katika shule.
Ameongeza kuwa kupitia Kongamano hilo lilianza Mei 7, 2025 litatoa fursa ya kuimarisha na kukuza uhusiano na ushirikiano katika nchi za Afrika sambamba na kuboresha sera na mifumo yake ya elimu ili kuendana na teknolojia, ubunifu na hususan matumizi ya akili mnemba.
Akieleza kuhusu eLearning Afrika, Mwanzilishi mwenza wa FIRCAD- Ghana, Dkt. Aida Opoku- Mensah amesema kuwa akili mnemba ina manufaa makubwa kwa maendeleo ya ikiwa ni pamoja na kutumika kutatua changamoto na kufanya shughuli kama binadamu.
Amesema akili mnemba imekuwa na umuhimu mkubwa katika maisha ya kila siku ya mwanadamu kwa kusaidia pia katika ufanyaji tafiti mbalimbali.
Amezungumzia utayari wa Afrika katika matumizi hayo na kusema kuwa baadhi ya nchi za Afrika zimekuwa na mwitikio wa haraka wa matumizi ya akili mnemba kuliko nyingine kutoka na uwekezaji wake.
Ametolea mfano Kenya (m-shule) na Nigeria tayari inatumia mifumo ya akili mnemba kwenye mifumo yake ya elimu na Tanzania kupitia ubongo kipindi kinachoelimisha na kuburudisha.
Amebainisha matumizi makubwa ya akili mnemba nchini China yamesaidia kukuza uchumi wake, aidha Afrika inatakiwa kuwekeza katika akili mnemba ili kusaidia katika sekta mbalimbali za elimu na miundombinu.
Kongamano na maonesho ya kila mwaka la eLearning Afrika , ambalo lilianzishwa mwaka 2005, ni tukio kubwa linalotoa fursa ya kubadilishana maarifa kwa elimu ya kidijitali, mafunzo na ujuzi katika Bara la Afrika.
http://KUSHIRIKIANA ZAIDI KIDIGITALI KATIKA SEKTA YA ELIMU_DKT.BITEKO .