Na, WAF-Dodoma
Serikali imesema Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Mloganzila zitaendelea kuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya kwa madhumuni ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuboresha ubora wa huduma sambamba na kutumika kama vituo vya mafunzo kwa wanafunzi wa vyuo vya Vikuu vya Dodoma na Muhimbili.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Thea Medard Ntara, Mei 07, 2025 kuhusu mpango wa kuzirudisha hospitali hizo chini ya vyuo husika, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema vyuo hivyo bado vinaendelea kuzitumia hospitali hizo kama sehemu ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa kada za afya.
“Vyuo vikuu vya Muhimbili na Dodoma vinaendelea kutumia Hospitali ya Mloganzila na Benjamin Mkapa kama hospitali za kufundishia, kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya katika kuhakikisha mazingira bora ya kitaaluma na huduma kwa wananchi,” amesema Dkt. Mollel.
Aidha, Dkt. Mollel amefafanua kuwa, usimamizi wa Wizara ya Afya umelenga kuimarisha mifumo ya huduma za afya huku ukihakikisha kuwa mahitaji ya vyuo vikuu vinavyotoa programu za afya yanaendelea kuzingatiwa.