Home LOCAL BUNGE LAAGIZA SERIKALI KUSAIDIA UPATIKANAJI WA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU KUPITIA NHC

BUNGE LAAGIZA SERIKALI KUSAIDIA UPATIKANAJI WA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU KUPITIA NHC

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

BUNGENI,  DODOMA 

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeielekeza Serikali kushughulikia kwa haraka changamoto ya upungufu wa nyumba za makazi kwa kuwawezesha wananchi kupata makazi bora na ya gharama nafuu kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Spika wa Bunge, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, alipokuwa akimtambulisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Hamad Abdallah, Bungeni Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu huyo alikuwa miongoni mwa wageni wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi.

Naibu Spika amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha Watanzania, hususan wenye kipato cha chini na kati, kupata makazi wanayoyaweza kwa gharama ili kuboresha hali zao za maisha.

“Bwana Hamad, ninachukua fursa hii kuwaelekeza mje na suluhisho la nyumba za gharama nafuu ili kusaidia kupunguza pengo la uhaba wa makazi nchini kupitia mpango wenu wa Samia Housing Scheme. Tunahitaji nyumba nyingi, bora na nafuu,” amesema Naibu Spika.

Aidha, amehimiza Shirika la Nyumba la Taifa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba katika mikoa mbalimbali, ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya makazi kwa wananchi.

Agizo hili linaendana na juhudi za Serikali za kuboresha maisha ya wananchi kupitia sekta ya makazi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa pamoja na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III).

Kwa upande wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lenyewe linaendelea kutekeleza mkakati wa kuhakikisha Watanzania wengi zaidi, hususan wa kipato cha chini na kati, wanapata nyumba bora na za gharama nafuu.

Kupitia mpango maalum wa Samia Housing Scheme, NHC imejipanga kujenga nyumba zinazolingana na uwezo wa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini. Lengo ni kupunguza pengo kubwa la mahitaji ya makazi, ambalo limekuwa changamoto kwa miaka mingi.

Mpango huu wa nyumba za gharama nafuu unazingatia:Ubora wa ujenzi unaokidhi viwango vya kitaifa. Bei rafiki kwa wananchi wa kipato cha chini na kati. Ujenzi katika maeneo yaliyo karibu na huduma za kijamii kama shule, hospitali na masoko na Utaratibu wa malipo unaomgusa mwananchi wa kawaida, ukiwemo mpango wa panga lipa au mkopo wa nyumba kwa urahisi wa marejesho.

Kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa sekta ya makazi, Shirika la Nyumba la Taifa

linaendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki ya msingi ya kuishi kwenye makazi salama, bora na yanayomuduwa.