Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi, ameanza ziara ya kikazi leo Mei 23, 2025, kwa ajili ya kukagua ujenzi wa minara ya mawasiliano katika Jimbo la Kibaha Vijijini, Mkoa wa Pwani.
Akizungumza wakati wa mapokezi yake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema mkoa huo una maeneo 27 makubwa ya uwekezaji wa viwanda, na ameiomba Wizara kuhamasisha wadau wa sekta binafsi kuwekeza katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa.
Kwa upande wake, Mhandisi Mahundi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina dhamira thabiti ya kuhakikisha maendeleo ya kidijitali yanafikiwa nchini kote. Ameahidi kuwa Wizara itaendelea kuchukua hatua madhubuti kushughulikia changamoto za mawasiliano katika Mkoa wa Pwani kwa suluhisho la kudumu.