Home LOCAL
Dkt. Ladislaus Chan’ga, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, akiwasilisha utabiri wa msimu wa Juni–Agosti, katika hafla iliyofanyika mapema leo Mei 22, 2025, jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam — Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) leo imetoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa hali ya joto, upepo na mvua kwa kipindi cha Juni hadi Agosti 2025 (msimu wa Kipupwe).
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chan’ga, ametoa tahadhari na ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Hali ya Joto: Baridi Kali Kutarajiwa Magharibi na Kusini
Kwa mujibu wa TMA, msimu wa JJA 2025 utatawaliwa na hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, baridi kali inatarajiwa hususan katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida na magharibi mwa Dodoma.
Mwezi Julai umetajwa kuwa ndio kipindi cha baridi zaidi, huku maeneo yenye miinuko yakitarajiwa kushuka chini ya nyuzi joto 6°C, hasa katika nyanda za juu kusini-magharibi.
Upepo: Kipupwe Kuambatana na Vipindi vya Upepo Mkali
TMA imetabiri upepo wa wastani kutoka Kusini Mashariki utakaotawala maeneo mengi, huku vipindi vya upepo mkali kutoka kusini (upepo wa kusi) vikitarajiwa hususan mwezi Juni na Julai, hasa katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na baadhi ya maeneo ya nchi kavu
Mwelekeo wa viwango vya joto la chini katika msimu wa Juni hadi Agosti, 2025
 
Mvua za Nje ya Msimu Zatarajiwa
Ingawa kwa kawaida Kipupwe huwa na ukavu, msimu huu vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu na Mara), pamoja na ukanda wa pwani na visiwa vya Unguja na Pemba.
Athari Zatarajiwa: Magonjwa, Vumbi na Upungufu wa Maji
TMA imeeleza kuwa baridi inaweza kupelekea ongezeko la magonjwa ya kuambukiza kama homa ya mapafu, na magonjwa ya mifugo katika baadhi ya maeneo. Pia, vumbi linalosababishwa na upepo linaweza kuathiri afya ya macho na kuongeza hatari ya magonjwa mengine.
Aidha, upungufu wa maji na malisho kwa mifugo unaweza kujitokeza kutokana na ukavu unaotarajiwa.
Wastani wa muda mrefu (1991-2020) wa viwango vya joto la chini kwa msimu wa Juni hadi Agosti.
Ushauri kwa Umma na Wadau
Dkt. Chan’ga amewashauri wananchi kuchukua tahadhari za kiafya, hasa katika maeneo yanayotarajiwa kupata baridi kali na vumbi. Wafugaji wanashauriwa kuzingatia ratiba za kuogesha mifugo na kufuata ushauri wa wataalamu, huku wakulima wakihimizwa kutumia maeneo oevu kwa kilimo cha mazao ya muda mfupi kama mbogamboga na viazi.
Watumiaji wa shughuli za baharini wametakiwa kufuatilia utabiri wa kila siku na angalizo kuhusu upepo mkali kwa usalama wao.
Ushauri kwa Umma na Wadau
Dkt. Chan’ga amewashauri wananchi kuchukua tahadhari za kiafya, hasa katika maeneo yanayotarajiwa kupata baridi kali na vumbi. Wafugaji wanashauriwa kuzingatia ratiba za kuogesha mifugo na kufuata ushauri wa wataalamu, huku wakulima wakihimizwa kutumia maeneo oevu kwa kilimo cha mazao ya muda mfupi kama mbogamboga na viazi.
Watumiaji wa shughuli za baharini wametakiwa kufuatilia utabiri wa kila siku na angalizo kuhusu upepo mkali kwa usalama wao.
 
Mwelekeo wa Mifumo ya Hali ya Hewa
Kwa mujibu wa TMA, joto la bahari linatarajiwa kuwa la wastani katika maeneo mengi ya tropiki, huku joto la juu ya wastani katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi likitarajiwa kudhoofisha upepo wa baridi kutoka kusini.
Angalizo
TMA itaendelea kufuatilia hali ya hewa na kutoa taarifa za mara kwa mara. Wananchi na wadau wanahimizwa kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 na mwezi kutoka TMA pamoja na tahadhari zinazotolewa kuhusu hali mbaya ya hewa.
Kwa taarifa zaidi, tembelea tma.go.tz au akaunti rasmi za TMA katika mitandao ya kijamii