Home LOCAL UCHAGUZI LAZIMA UFANYIKE KWA KUWA UPO KWA MUJIBU WA KATIBA –DKT. NCHIMBI

UCHAGUZI LAZIMA UFANYIKE KWA KUWA UPO KWA MUJIBU WA KATIBA –DKT. NCHIMBI

SONGEA

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 utafanyika kama ilivyoelekezwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akisisitiza kuwa hakuna mtu binafsi, chama au mamlaka yoyote, hata ya juu serikalini, inayoweza kuzuia kufanyika kwake.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Akizungumza katika Mkutano Mkuu Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) unaofanyika leo Ijumaa Aprili 04, 2025 mjini Songea, Dkt. Nchimbi amesema kuwa utaratibu wa uchaguzi nchini ni wa kikatiba na umeendelea kuzingatiwa tangu mwaka 1960.

“Nchi yetu ina utaratibu wa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano. Hakuna raia yeyote, hata Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu mwenye mamlaka ya kusema uchaguzi hautafanyika,” alisema.

Ametoa kauli hiyo kufuatia mjadala unaoendelea juu ya ushiriki wa vyama vya siasa, hasa CHADEMA, katika uchaguzi huo. 

“Niwahakikishie Watanzania kuwa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwaka 2025 utafanyika kama kawaida,” aliongeza.

Dkt. Nchimbi amewakumbusha wananchi kuwa, ingawa kila raia ana haki ya kugombea, hakuna chama kinachoweza kulazimishwa kushiriki uchaguzi. 

“Zimeanza kusikika sauti za baadhi ya wana CCM na wananchi wakishinikiza CHADEMA iingie kwenye uchaguzi. Ni haki yao kususia,” alisema.

Akiwazungumzia viongozi wa CHADEMA akiwemo Tundu Lissu, Dkt. Nchimbi amesema: 

“Ndugu zangu wa CHADEMA, uchaguzi huu si wa mwisho. Kuna uchaguzi wa mwaka 2030, 2035, 2040, 2045 hadi 2050. Wasipoupata huu, wataupata ule mwingine.”

Aidha, amekemea tabia ya kuwakejeli au kuwalazimisha wapinzani kushiriki uchaguzi.

 “Kukaa kuwasema sema CHADEMA ni kinyume cha sheria na katiba. Mtu yeyote asiwalazimishe CHADEMA kuingia kwenye uchaguzi,” alisisitiza.

Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Katiba inaruhusu uchaguzi kufanyika hata kwa chama kimoja pekee, na kwamba kila raia ana haki ya kuchagua hata kama hataki kugombea. 

“Ukikosa haki ya kuchaguliwa, unapata haki ya kuchagua. Katika haki mbili, unapata moja na unakuwa umejitendea haki kama raia wa Tanzania,” alisema Dkt. Nchimbi.