Home ENTERTAINMENTS TANZANIA YAJIPANGA KWA AJILI YA MKUTANO WA FUTURE READY NA WIKI YA...

TANZANIA YAJIPANGA KWA AJILI YA MKUTANO WA FUTURE READY NA WIKI YA UBUNIFU TANZANIA 2025.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara (katikati) akizungumza kwenye mdahalo uliofanyika wakati wa kutangaza msimu mpya wa Wiki ya Ubunifu sambamba na mkutano wa Future Ready Summit mwaka 2025. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire na muongozaji wa mdahalo huo Hilda Phoya.

…………. 

Dar es Salaam, Tanzania – Ubunifu unachukua nafasi ya kipekee mwezi Mei wakati Tanzania ikijiandaa kwa ajili ya Wiki ya Ubunifu Tanzania maarufu kama ‘Innovation Week Tanzania’ (IWTz) kwa mwaka 2025, jukwaa shirikishi linaloangazia kuleta suluhisho kwa maendeleo endelevu. 

Tukio hili litafanyika kuanzia tarehe 12 hadi 16 Mei 2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), likiratibiwa kwa ushirikiano kati ya Vodacom Tanzania PLC, UNDP Tanzania kupitia programu yake ya FUNGUO na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH).

Ikiwa na kaulimbiu ya mwaka huu, “Ubunifu kwa Mustakabali Jumuishi na Wenye Ustahimilivu,” IWTz 2025 inalenga kushughulikia changamoto kuu zinazolikumba taifa ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana, pengo la ujuzi wa kidijitali na maendeleo ya miji kwa kutumia nguvu ya ubunifu wa ndani ya nchi pamoja na mbinu bora za kimataifa. Mwaka huu pia, tukio hili litajumuisha Mkutano wa Vodacom Future Ready Summit (FRS2025), ambao utalenga mageuzi ya miji ya Tanzania kupitia ubunifu, miundombinu ya kidijitali na sera jumuishi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, alisisitiza umuhimu wa maendeleo yanayoendeshwa na teknolojia na ushirikiano wa sekta mbalimbali: “Vodacom si mtoa huduma wa mawasiliano tu; sisi ni kichocheo cha maendeleo. Dhamira yetu ya kuendeleza ubunifu inaonekana katika kila mipango yetu — kutoka Code Like a Girl, Digital Accelerator hadi Future Ready Summit. Kupitia ushirikiano wetu na UNDP, COSTECH na wadau wengine, tunalenga kuchochea mijadala itakayounda Tanzania ijayo — Tanzania ya kidijitali, jumuishi na yenye ustahimilivu. Jukwaa hili linahusu kubadilisha mawazo na mitazamo, na kuwapa Watanzania zana za kuendesha mabadiliko ndani ya jamii zao.”

Kwa Vodacom, mkutano huu ni mwendelezo wa dhamira yake pana ya “kuunganisha watu kwa ajili ya mustakabali bora.” Kupitia ubunifu kama vile M-Pesa, M-Pawa, VodaBima, M-Koba na majukwaa ya elimu ya kidijitali, kampuni hiyo imeonesha jinsi sekta binafsi inaweza kuongoza katika kutoa fursa sawa kwa wote.

Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara, alisisitiza dhamira hiyo akisema: “Ubunifu si anasa; ni hitaji la maendeleo jumuishi. Kupitia programu yetu ya FUNGUO, tunalenga kuwawezesha vijana, wanawake na biashara changa kote nchini Tanzania. Ushirikiano wetu na Vodacom na COSTECH unatuwezesha kufanikisha maono haya kwa kiwango kikubwa zaidi. IWTz 2025 itaonesha ubunifu wa Tanzania kwa dunia nzima, ikichochea mawazo mapya, ushirikiano na matokeo chanya.”

Mwaka huu utaambatana na maonesho, warsha, midahalo ya wawekezaji na hafla za mitandao ya kijamii na biashara. Pia tutatumia fursa hii kama jukwaa la kuangazia biashara changa za ndani, uvumbuzi wa sera na mchango wa sayansi na teknolojia katika kubadili sekta kama vile elimu, afya, kilimo na fedha.

Akizungumza kwa niaba ya serikali, Dk. Athumani Mgumia, Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo na Uhawilishaji wa Teknolojia kutoka COSTECH, alisema: “COSTECH imedhamiria kuendeleza tafiti na ubunifu unaoendana na dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050. Wiki ya Ubunifu 2025 ni jukwaa muhimu kwa sekta ya umma na binafsi katika kuunda kwa pamoja suluhisho zinazojibu mahitaji halisi ya wananchi na kuiweka Tanzania kuwa kinara wa ubunifu katika ukanda wa Afrika.”

Mbali na tukio kuu litakalofanyika Dar es Salaam, shughuli za uhamasishaji na maonesho katika vyuo vikuu mbalimbali zinahusisha wabunifu, viongozi katika jamii na wanafunzi nchini kote—hii ikiwa ni kuhakikisha ubunifu hauishii mijini tu bali unawafikia wananchi walioko maeneo ya pembezoni. Shughuli hizi zinafanyika pia katika vyuo vikuu mbalimbali vikiwemo State University of Zanzibar (SUZA), Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dar es Salaam Institute of Technology (DIT) kwa jijini Dar es Salaam na tawi la Mwanza, Chuo Kikuu cha Iringa na Mbeya University of Science and Technology (MUST).

Ikiwa imebaki wiki chache tu kabla ya kuanza kwa IWTz 2025, hamasa na matarajio yanazidi kuongezeka. Tukio hili si mkutano wa kawaida—ni harakati ya kuibua mustakabali mpya wa maendeleo unaoongozwa na Watanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliojitolea kufungua fursa katika kila kona ya nchi.

 http://TANZANIA YAJIPANGA KWA AJILI YA MKUTANO WA FUTURE READY NA WIKI YA UBUNIFU TANZANIA 2025.