Home LOCAL SONGEA WAOMBA UCHUNGUZI WA MAGONJWA YA SARATANI UWE ENDELEVU.

SONGEA WAOMBA UCHUNGUZI WA MAGONJWA YA SARATANI UWE ENDELEVU.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na Mwandishi wetu

Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wameiomba Wizara ya Afya kupitia Taasisi ya Saratani (Ocean Roads) na kampeni ya huduma za mkoba za Dkt Samia Suluhu Hassan ambazo zinatolewa bure na madaktari bingwa wabobezi kuwa endelevu.

Aidha timu ya wataalamu kutoka Taasisi ya Saratani Oceanroad wameweka kambi ya siku saba katika Hospitali Ya Rufaa ya Mtakatifu Joseph Peramiho kwa ajili ya matibabu na uchunguzi wa magonjwa hayo.

Kelvin Ponera, ni mmoja wa wanufaika wa uchunguzi huo ambapo anasema huduma zinazotolewa katika kambi ya Mkoba ya Samia Suluhu Hassani ni muhimu kuwa endelevu.

“Tunaomba Wizara na serikali yetu kuona haja ya huduma hizi kuwa endelevu kwa lengo la kuwapunguzia ghalama wananchi lakini pia kupata mapema taarifa za ugonjwa wa saratani hali ambayo itapunguza athari zake na vifo,”amesema.

Naye mnufaika John Bosco, ambaye ni mkazi wa Songea Mjini ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuwaleta madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa ya saratani ambao wamekuwa ni msaada katika uchunguzi na ushauri wa namna bora ya kuepuka magonjwa hayo.

“Baadhi ya wananchi waliojitokeza kufanyiwa uchunguzi na baadae kupatiwa matibabu wengi wetu ni wenye maisha ya kwaida hivyo hatua ya wataalamu hawa kuweka kambi maeneo ya karibu imetupunguzia gharama ya kupata huduma,”amesema.

Kwa upande wa Meneja wa huduma za uchunguzi na Mkurugenzi wa kinga kutoka Ocean Roads, ambaye ni Daktari bingwa Maguha Stephano,
amesema lengo la kampeni ya mkoba ya Samia Suluhu Hassani ni kugundua hatua za awali za saratani ambazo zinatibika, kutoa elimu ya uelewa wa chanzo cha magonjwa hayo na namna bora ya kujikinga na kutoa tiba kwa wagonjwa wanaogundulika.

Akiongoza jopu la wabobezi wa magonjwa ya saratani, Mkurugenzi Mtendaji wa Ocean Roads Dkt Diwani Msemo, amesema hatua hiyo imefikiwa kutokana na maagizo, maono ya Rais Dkt Samia ya kuhakikisha taasisi inachukua hatua na vifo vinavyotokana na saratani vinapungua nchini.

Mwisho