Matukio mbalimbali katika uzinduzi wa Kitabu cha “Mwalimu Julius Kambarage Nyerere: Photographic Journey” uliofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 26 Aprili, 2025.
……………..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuenzi maisha ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kufanya kazi kwa bidii ili kujenga Taifa na kujiletea maendeleo.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Shirika B. Nyanga imesema Rais Dkt. Samia amesema hayo leo wakati akizindua kitabu cha ’Mwalimu Julius Nyerere: Photographic Journey’ katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino. Uzinduzi wa kitabu hiki ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Rais Dkt. Samia amesema kitabu hiki kimebeba masuala mengi kuhusu maisha ya Hayati Mwalimu Nyerere ambae aliacha alama isiyofutika kwenye historia ya nchi kwa kuwahimiza Watanzania kuwa wamoja, kushikamana na kufanya kazi kwa bidii kwa maendeleo ya nchi yetu.
“Nilipotakiwa kuandika dibaji na maneno ya kufunga ya kitabu hiki sikusita. Nimefurahi kuzinduliwa leo sambamba na kutoa nishani kwa viongozi walioutumikia Muungano wetu … Mwalimu alikuwa kinara wa falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea na Maendeleo Jumuishi au Maendeleo ya Watu. Falsafa hiyo imeendelea kuwa msingi wa uongozi wetu”. amesema Rais Dkt. Samia.
Rais Dkt. Samia pia amesema Hayati Mwalimu Nyerere aliamini kuwa nguvu ya Tanzania ipo kwenye umoja na mshikamano wa watu wake na alisimamia kwa uthabiti mkubwa yale aliyoyaamini. Kitabu kinatukumbusha namna alivyojenga Taifa jumuishi bila ubaguzi wa rangi, kabila au majimbo hivyo kuwezesha watu tofauti kutoka sehemu tofauti kufanya kazi pamoja.
Kipekee Rais Dkt. Samia amemtaja Mwalimu Nyerere kuwa ni kiongozi aliyeamini katika wanawake katika kipindi ambacho wanawake hawakuthaminiwa, aliamini wanawake wanapopata nafasi na kutoa mchango wao wanafanya mambo makubwa kwa jamii.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amegusia umuhimu wa kutunza kumbukumbu za viongozi kwa mustakabali wa kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na viongozi wawili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, ambapo aliweka wazi kuwa changamoto za Muumgano zimetatuliwa kwa kuenzi falsafa za waasisi wake walioamini katika umoja na mshikamano.
Kitabu hiki ni sehemu ya juhudi ya Serikali ya Awamu ya Sita kuenzi na kutunza kumbukumbu za viongozi waliolitumikia taifa kwa nyakati tofauti.
Akizungumzia utekelezaji wa maono ya Mwalimu Nyerere, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Mwalimu Nyerere alitaka kuwawezesha wahitimu kujitegemea, ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Sita imeanza kutekeleza Sera ya Elimu iliyoboreshwa ili wahitimu waweze kuajiriwa na kujiajiri.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amewaasa Watanzania kudumisha amani kwani migogoro na uvunjifu wa amani na mivutano haitaleta maendeleo ya kweli, hivyo amewataka wananchi washikamane kujenga Taifa ili kuleta ustawi.
Awali, Rais Dkt. Samia alitunuku Nishani za Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Pili na Nishani za Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Tatu kwa Viongozi 8 ambao katika kipindi cha uongozi wao walijitoa bila kusita kudumisha Muungano na wameendelea kuonesha maadili bora na kuwa mfano wa kuigwa hata baada ya utumishi wao.
Viongozi waliotunukiwa Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Pili ni: Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Mohamed Ali Shein; Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Idd; Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa; Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda; Spika Mstaafu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Pandu Ameir Kificho; Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Profesa Ibrahim Hamisi Juma na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Hayati Balozi John William Kijazi.
Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Tatu imetunukiwa kwa Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Ndg. Philip Japhet Mangula.