Home LOCAL OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI MBIONI KUKAMILISHA ZOEZI LA UREKEBU WA...

OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI MBIONI KUKAMILISHA ZOEZI LA UREKEBU WA SHERIA

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha zoezi la Urekebu wa Sheria mbalimbali nchini.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Hayo yameelezwa na Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius Njole wakati akizungumza katika kipindi cha televisheni cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC, tarehe 11 Aprili, 2025.

Mwandishi Mkuu wa Sheria, amesema kuwa zoezi la Urekebu wa Sheria ni moja ya majukumu ya msingi ya kikatiba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, zoezi la urekebu linahusisha kupitia sheria za nchi kwa lengo la kujumuisha marekebisho mbalimbali yaliyofanyika katika nyakati tofatui katika sheria husika.

Aidha, Bw. Njole amesema kuwa lengo kuu la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya zoezi la urekebu ni kuingizia marekebisho yaliyofanyika katika sheria mbalimbali na kuwawezesha pamoja na kuwarahisishia watumiaji wa sheria, kutumia sheria ambazo zipo na zinazokwenda na wakati.

*“Kwa kutambua umuhimu wa kuwa na sheria zinazokwenda na wakati Bunge la Jamhuri lilitunga sheria mahususi inayoitwa ya Urekebu wa Sheria Sura ya 4, inayompa mamlaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia kwa Mwandishi Mkuu wa Sheria kutekeleza zoezi la urekebu wa sheria.”* Amesema Bw. Njole

Mwandishi Mkuu wa Sheria amesema kuwa zoezi la urekebu wa sheria linalotarajiwa kuzinduliwa hivi karibu linajumuisha jumla ya sheria kuu 446, ambapo zoezi hilo limefanyika kwa kuwatumia wataalamu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

*“Zoezi hili la Urekebu wa sheria linahusisha jumla ya sheria Kuu za Nchi 446, pamoja na sheria ndogo takribani 30,000.”* Amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria.

Katika hatua nyingine, Mwandishi Mkuu wa Sheria, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa jitihada mbalimbali ilizochukua katika kuona umuhimu wa kuwa sheria zinazokwenda na wakati, ambapo amesema kuwa Serikali imekuwa ikiendelea kujenga uwezo kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuongeza fedha kwa ajili ya kufanya urekebu pamoja na kuongeza idadi ya Waandishi wa Sheria ili kuwezesha zoezi hili kufanyika kwa wakati.

Tunaipongeza Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikiwezesha upatikanaji wa raslimali fedha na rasilimali watu ambapo kwasasa zoezi hili tunalifanya kwa wakati na kutumia wataalamu wa ndani.” Amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria.