Home LOCAL MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA MAWAKILI KUJIVUNIA TAALUMA YAO

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA MAWAKILI KUJIVUNIA TAALUMA YAO

:Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, akizungumza na mawakili wa serikali kwenye mkutano  mkuu wa chama cha mawakili wa serikali unaofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma kuanzia leo Aprili 14, 2025.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel Maneno akimkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari ili kuzungumza na mawakili wa serikali katika mkutano huo.

…………..

Na Mwandishi Wetu – Dodoma

Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, amewataka mawakili wa serikali nchini kujivunia taaluma yao huku wakihakikisha wanachagua viongozi wenye uwezo mkubwa wa kuendeleza na kutekeleza malengo ya Chama cha Mawakili wa Serikali.

Akizungumza leo katika Mkutano Mkuu wa Chama hicho unaofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, Mhe. Johari alisema mkutano huo ni fursa muhimu kwa mawakili wote wa serikali kujadili mustakabali wa chama chao pamoja na maendeleo ya sekta ya sheria kwa ujumla.

“Huu ni mwaka wa tatu tangu kuanzishwa kwa chama hiki. Ni fursa adhimu kukutana na mawakili wote wa serikali na kujadili namna ya kukijenga chama kuwa chenye nguvu na ushawishi,” alisema.

Mhe. Johari alibainisha kuwa lengo kuu la mkutano ni kutoa nafasi kwa wanachama kujadili changamoto, mafanikio na mikakati ya kuimarisha utendaji wao kwa kuzingatia ukuaji wa taaluma na mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa uchaguzi wa viongozi wenye fikra pana na dira ya maendeleo, watakaoshirikiana na uongozi wa juu wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kuleta mabadiliko chanya ndani ya chama.

Akizungumzia kaulimbiu ya mkutano huo isemayo “Utawala wa Kisheria katika Utekelezaji wa Majukumu ya Serikali ni Nguzo Muhimu katika Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”, Mhe. Johari alisema inatoa mwelekeo sahihi wa jinsi sekta ya sheria inavyopaswa kujipanga kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050.

“Dira hii ni ya kila mmoja wetu. Kila mdau anapaswa kuisoma na kuielewa vizuri ili kutekeleza wajibu wake kwa weledi,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno, aliwahimiza mawakili wa serikali kote nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi bila woga, na kuzingatia maelekezo kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Hakuna sababu ya kuogopa kutoa ushauri wa kisheria au kufika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo ni ofisi yetu sote. Tuilinde na tuimarishe umoja wetu kupitia chama chetu,” alisema Maneno.

Aliongeza kuwa mshikamano, ushirikiano na mashauriano ndani ya chama vitasaidia kufikia malengo ya pamoja na kumuunga mkono Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu ya kisheria ya serikali.