Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa mabadiliko yaliyofanyika kwenye sekta ya afya ikiwemo uwekezaji kwenye miundo mbinu na ubora wa huduma ndio mabadiliko chanya wanayohitaji Watanzania.
Dkt. Mollel ametoa kauli hiyo leo Aprili 4, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya afya nchini ambayo yanaendelea kufanyika kwa mafanikio makubwa.
“Tanzania inahitaji mabadiliko ili kufanikisha maendeleo endelevu. Maendeleo ya sekta ya afya ni kielelezo tosha cha dhamira ya Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi, mabadiliko wanayohitaji Watanzania ni maendeleo kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya afya,” amesema Dkt. Mollel.
Dkt. Mollel ameeleza kuwa kwa mara ya kwanza, Tanzania inaadhimisha wiki ya afya ikiwa imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi, vifo vya mama na mtoto pamoja na idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa matibabu.
Aidha, Dkt. Mollel amebainisha kuwa moja ya mafanikio makubwa ya sekta ya afya ni kupungua kwa vifo vinavyosababishwa na saratani kwa asilimia 78 ambapo hatua hiyo imechangiwa na maboresho katika mfumo wa uchunguzi wa mapema wa magonjwa hayo, hali iliyowezesha utambuzi wa saratani ambazo awali zilikuwa haziwezi kugundulika mapema.
“Sasa Tanzania tuna uwezo wa kugundua saratani ambazo awali zilitarajiwa kuonekana baada ya miaka 10 ijayo. Hii ni hatua kubwa kwa taifa letu,” amesema Dkt. Mollel.