Home LOCAL DKT NCHIMBI AAGIZA WAKALA WA MBEGU ASA KUONGEZA UZALISHAJI

DKT NCHIMBI AAGIZA WAKALA WA MBEGU ASA KUONGEZA UZALISHAJI


Mbunge wa Jimbo na Namtumbo Mkoani Ruvuma Vita Kawawa kushoto,akiwaongoza Wabunge wenzake wa Mkoa wa Ruvuma Jonas Mbunda(Mbinga Mjini)Hassan Kungu(Tunduru mjini na Jacline Msongozi Viti maalum kucheza muziki wa Singeli wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapnduzi Dkt Emanuel Nchimbi Wilayani Namtumbo jana.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!


Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dkt Emanuel Nchimbia,kipkea kadi za Chama cha ACT-Wazalendo kutoka kwa baadhi ya Wanachama wa ACT na CUF walioamua kurudisha kadi za vyama vyao na kujiunga na Chama cha Mapinduzi jana.

Namtumbo

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi  Dkt Emanuel Nchimbi,ameutaka Wakala wa mbegu kilimo nchini(ASA),kuongeza uzalishaji wa mbegu ili wakulima wengi wanufaike na uwekezaji unaofanywa na Serikali kwenye sekta ya kilimo.

Dkt Nchimbi,ameiagiza ASA kufungua ofisi zake wilayani Namtumbo ili wakulima waweze kupata mbegu kwa urahisi na bei nafuu zaidi, hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani.

Dkt Nchimbi ametoa maagizo hayo jana,alipokuwa akizungumza na mamia ya Wananchi wa Wilaya ya Namtumbo akiwa katika ziara ya siku tano kutembelea Mkoa wa Ruvuma.

Amewapongeza Wananchi wa Wilaya ya Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma kwa kazi nzuri ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, hata hivyo amewasisitiza waongeze bidii ili waweze kujikwamua na umaskini  kupitia shughuli zao za kilimo.

Alisema,jitihada zao zimeifanya Wilaya ya Namtumbo kushika nafasi ya pili kiuzalishaji  katika Mkoa wa Ruvuma na Mkoa huo kuongoza kitaifa kwa uzalishaji na kuendelea kuwa ghala la Taifa la Chakula.

“Heshima ya binadamu ni kufanya kazi ili aweze kujitegemea,ndiyo maana kila mmoja anataka kufanya kazi ili kuepuka  aibu ya kuwa ombaomba kwa watu wengine,nawapongeza sana Wananchi wa Namtumbo na Ruvuma kwa ujumla kwa kazi nzuri mnazofanya,Serikali ya Chama cha Mapinduzi lazima iko nyuma yenu”alisema.

Nchimbi,amewaomba Watanzania kumuunga Mkono Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya awamu ya sita kwa kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo na kujivunia kuwa na Rais ambaye ni kioo kwa Mataifa mengine Duniani.

“Rais Samia Suluhu Hassan,amefanya mambo mengi mazuri ambayo ni mfano wa kuigwa na Mataifa mengine Ulimwenguni ikiwemo suala la upatikanaji wa huduma ya maji na afya ambazo zimepunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto” alisema.

Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi  kutoa kiasi cha Sh.bilioni 7.798 ili kuboresha huduma ya majisafi na salama katika Mji wa Namtumbo.

Kawawa ameipongeza Serikali kwa kuruhusu kuendelea kwa shughuli za utafiti wa mradi wa Uran na  kueleza kuwa,mradi huo utakapoanza kufanya kazi Serikali na Halmashauri ya Wilaya itapata mapato.

Alisema,katika kipindi cha miaka minne  Wilaya ya Namtumbo imepokea fedha zilizofanikisha kujenga shule tano za Sekondari ikiwemo shule ya Sekondari ya Dkt Samia Suluhu Hassan kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 4,shule ya Sekondari Msisima na Hanga ambazo kila moja imegharimu Sh.milioni 600.

Kwa mujibu wa Kawawa,katika kipindi cha miaka minne Serikali ya awamu ya sita imetoa zaidi ya Sh.bilioni 6.147 kujenga zahanati mpya 15 katika vijiji mbalimbali,vituo vya afya,kununua dawa na vifaa tiba ambavyo vimesaidia wananchi wa kupata huduma bora za afya na kupunguza kwa vifo vya mama na mtoto.

Kawawa, amemuomba Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Taifa, kuikumbusha Serikali kuhusu kutekeleza ahadi ya kujenga barabara ya Mtwarapachani-Nalas-Tunduru mjini na barabara ya Lumecha-Hanga- Malinyi  hadi Ifakara mkoani Morogoro kwa kiwango cha lami.

Kwa mujibu wa Kawawa,barabara hizo zikijengwa kwa  lami zitachochea kukua kwa uchumi wa Wananchi wa Namtumbo kwa kuwa zinapita kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara.

Kwa upande wake Mwanachama wa Chama hicho Mchungaji Peter Msigwa alisema,Chama hicho kimekuwa mfano mzuri kwa jamii ya Watanzania kutokana na kuboresha maisha ya watu wake,kufikisha huduma za kijamii na kuweka sera nzuri ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo.