Aliyekuwa Katibu wa Sekretarieti ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Julius Mwita, amemtaka Mwanaharakati Maria Sarungi, kujitokeza hadharani na kueleza ikiwa ni mwanachama wa Chadema kwa kuonesha kadi yake ya uanachama wake ndani ya Chadema.
Mwita ambaye amezungumza na wanahabari Jijini Dar Es salaam leo Aprili 3, 2025, siku moja mara baada ya kuvuliwa nafasi yake ndani ya Chadema, amefikia hatua hiyo mara baada ya kuhoji uhalali wa Maria Sarungi kuhoji maamuzi ya Chama, akimtaja kuwa kama Mwenye Chama kwa namna ambavyo amekuwa akijihusisha moja kwa moja na maamuzi ya vikao halali vya Chadema.
“Kuna mtu anaitwa Maria Sarungi, kikao kimeitishwa na Katibu Mkuu, mimi sijui hata kama Maria ni mwanachama wa Chadema, mimi ni mwanachama na kadi yangu ni platnums, yeye aje atuambie kadi yake ni namba ngapi. Maria anapost Twitter anahoji kikao cha watia nia kimeitishwa na nani kwasababu viongozi wote wakuu wapo field, serious? Who is she?mtu anaishi Nairobi, anaogopa hata kuja kumzika baba yake leo anahoji mambo ya chama?” Amesema Mwita
Katika Hatua nyingine, Mwita kutokana na Mawasiliano yao yaliyovuja yakitokea kwenye kundi sogozi la WhatsApp, alionekana akiandika mara kadhaa “huyo Boss wao” ambapo amekiri kuwa aliyekuwa akimzungumzia kama “Boss wao” sio Mwenyekiti wa Chama Mhe. Tundu Lissu bali ni Maria Sarungi ambaye amemtaja kama Mtu mwenye rimoti ya kuendesha Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.