Home LOCAL BUMBULI WAMTAKA JANUARY MAKAMBA AJIUZULU UBUNGE, WADAI HANA TIJA KWA JIMBO

BUMBULI WAMTAKA JANUARY MAKAMBA AJIUZULU UBUNGE, WADAI HANA TIJA KWA JIMBO

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

 Dar es Salaam 

Wananchi wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga wamemtaka Mbunge wao, January Makamba, kujiuzulu nafasi hiyo kwa madai ya kushindwa kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni.

Wakizungumza na wanahabari leo, Aprili 2, 2025, jijini Dar es Salaam, wananchi hao wamesema kuwa licha ya kumpa kura Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu ujao, hawako tayari kumpigia kura tena Makamba kwa nafasi ya ubunge.

“Miaka 15 ya Makamba imekuwa mateso kwa Bumbuli,” wamesema wananchi hao, wakibainisha changamoto nyingi zinazodhoofisha maendeleo yao.

Changamoto Zinazowakabili Wananchi

Miongoni mwa matatizo waliyoeleza ni hali mbaya ya miundombinu, hasa barabara, ambayo imeathiri sekta ya kilimo. Bw. Eric Edward kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli amesema walitarajia Makamba kutatua changamoto ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa chai, lakini hali imeendelea kuwa mbaya.

“Kiwanda cha Mponde kilianza kwa nguvu lakini sasa thamani ya chai imeshuka. Wakulima wanahangaika kusafirisha mazao kwa bajaji kwenye barabara mbovu,” alisema Edward.

Naye Elias Kamute alizungumzia tatizo la maji, akisema: “Bumbuli ina maji mengi, lakini hadi leo tunapata mgao. Ahadi zimekuwa nyingi, lakini utekelezaji hakuna kwa zaidi ya miaka 15.”

Kwa upande wake, Khalid Kijazi alisema Makamba hana uhusiano wa karibu na wananchi wa Bumbuli, akidai kuwa “Ni kama mtalii wa nje na Dar es Salaam badala ya kushughulikia changamoto za jimbo lake.”

“Tunahitaji kiongozi mpya kwa sababu Makamba ameshindwa kutimiza wajibu wake,” alisema Ayubu Radhid, akieleza jinsi miundombinu mibovu imeathiri wakulima wa eneo hilo.

Merry Gendo naye alieleza kusikitishwa na kutotimizwa kwa ahadi za mikopo kwa wajasiriamali wadogo, huku akidai Makamba aliwahi kusema “Wananchi wa Bumbuli hawahitaji maendeleo bali pesa za dagaa.”

Katika sekta ya afya, Iddy Amiri alisema huduma duni za matibabu na uhaba wa madaktari ni matatizo makubwa, huku elimu nayo ikidorora kutokana na ukosefu wa walimu na miundombinu duni.

“Makamba aliahidi kuboresha elimu, lakini hakuna kilichotekelezwa. Tunahitaji mbunge mpya atakayeleta maendeleo ya kweli,” alisema.

Wananchi hao wamesisitiza kuwa ni wakati wa mabadiliko, wakimtaka January Makamba kuachia ngazi ili nafasi hiyo ichukuliwe na mtu mwingine mwenye uwezo wa kuwatumikia kwa ufanisi.