Na WAF – Dodoma
Wauguzi, Wakunga na Watoa huduma za afya, wameagizwa kuendelea kubeba dhamana kubwa katika kuwapatia huduma bora Watanzania kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ilivyowekeza katika sekta ya afya.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Festo Dugange wakati akimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Wauguzi Viongozi Machi 26, 2025 Jijini Dodoma.
“Ninawaelekeza Wauguzi Viongozi wa ngazi zote kuimarisha usimamizi wa utoaji wa huduma bora ili wananchi wote wapate huduma bora na kwa Usawa, Tunatambua kuwa wauguzi wanafanya kazi nzuri sana japo kuna baadhi yenu wachache wanaharibu sifa nzuri ya wauguzi kwa kufanya makosa mbalimbali yanayoweza kuepukwa,” amesema Dkt. Dugange.
Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa ujumla inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wauguzi kwa watanzania na kwamba wao ni kiungo muhimu cha maendeleo.
Amefafanua kuwa Serikali, imewekeza katika ngazi ya msingi pekee jumla ya Shilingi Trilioni 1.3 katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake sambamba na kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya ya msingi.
Katika Uwekezaji huu Mhe. Rais amezingatia usawa katika maeneo ya mijini na vijijini, makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na walemavu, wazee, wanawake, vijana na watoto pamoja na kununua vifaa na vifaa tiba kwenye zahanati, vituo vya Afya na hospitali nchini kote.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amepongeza ushiriki wa wauguzi katika mapambano ya magonjwa ya mlipuko hususani katika kuudhibiti ugonjwa wa Marburg nchini.
“Tunapozungumzia wauguzi na wakunga ni rasilimali watu ambayo inafikia asilimia 60 ya wataalam wote wa sekta ya afya na majukumu mnayofanya yanafikia asilimia 80. Huduma zote haziwezi kuboreka bila kuwa na rasilimali watu, inahitajika kuwa na watu wenye uwezo, weledi na ujuzi kama ninyi,” amesema Dkt. Magembe.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Bi. Ziada Sellah ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mambo mbalimbali ya kada hizo kwani ilivyo sasa siyo sawa na miaka 10 iliyopita.
http://WAUGUZI, WAKUNGA ENDELENI KUBEBA DHAMANA KAMA SERIKALI ILIVYOWEKEZA