Na Khadija Kalili , Michuzi TV
MAKAMU MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira, amesema vyama ya ukombozi Kusini Mwa Afrika viendeshwe Kwa kuzingatia mahitaji ya wakati huu bila kusahahu shabaha ya kuanzishwa kwake.
Amesema kuwa vyama hivyo vilipigania uhuru kuzikomboa jamii za waafrika ambazo ndani yake ina vizazi vilivyopo na vitakavyokuja.
Wassira amesema hayo leo tarehe 3 Februari 2025 alipokuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo kwa viongozi vijana kutoka vyama rafiki vya ukombozi Kusini mwa Afrika iliyofanyika lkatika Shule ya Uongozi ya Julius Nyerere, Kibaha Mkoani Pwani.
Vyama hivyo ni FRELIMO (Msumbuji), MPLA (Angola), ANC (Afrika Kusini), SWAPO (Namibia), ZANU-PF (Zimbabwe) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Tanzania ambapo katika mapambano ya ukombozi vilishirikiana kwa karibu na Chama Cha Kikomunisti Cha China (CPC).
Mhe.Wassira amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha vyama hivyo ambapo anaamini mifumo ya siasa inabadilika kutoka chama kimoja kwenda vyama vingi na lazima kutafuta mbinu ambayo itavifanya vyama hivyo kujiimarisha kutoka chini, visiwe vyama vya watu wachache hatua ambayo inalenga kuhakikisha vinaendelea kuongoza nchi zao.
“Mbinu za kuongoza nchi zao ni kuhakikisha mabadiliko yoyote ya dunia hayayumbishwi lakini pamoja na kwamba ni lazima washirikiane na dunia nyingine wasifanye dunia ikawa badala ya shabaha yao, maana duniani hapa kuna mambo yake vilevile.
“Vyama hivi shabaha yake ni ya muda mrefu ambayo ni kuona dunia ina maisha bora kwa watu wake ambao wanazaliwa kila siku, hata kama kuna mabadiliko mengi yanatokea shabaha inabaki ile ile kuona watu wetu katika nchi hizi wanapata maisha mazuri na hii ndiyo shabaha ya msingi na haina mwisho, huwezi kusema maisha sasa yametosha,” amesema amesema Wassira.
Akizungumzia nafasi ya vijana, amesema ndiyo warithi halali wa vyama hivyo, hata yeye alikuwa kijana na hiyo inamaanisha kuwa hakuna maendeleo bila kijana.