Home LOCAL WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI NA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI NA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na FARIDA MANGUBE, MOROGORO

Waandishi wa habari wametakiwa kuendelea kuandika habari kwa kuzingatia ueledi, maadili, na misingi ya taaluma, huku wakilinda faragha na utu wa mtu binafsi.

Mkurugenzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia, ameyasema wakati akifungua warsha ya siku moja kuhusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa Jukwaa la Wahariri wa Vyombo vya Habari Tanzania TEF iliyofanyika Mjini Morogoro.

Amesema kwa dunia ya sasa inayosukumwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ulinzi wa taarifa binafsi ni jambo la msingi, hasa ikizingatiwa kuwa taarifa nyingi husambazwa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii.

Dkt. Mkilia amesema kuwa Tume hiyo inatambua mchango mkubwa wa wahariri na waandishi wa habari katika kulinda taarifa binafsi, kwani wao ni nguzo muhimu katika kuhakikisha faragha ya mtu inaheshimiwa kwenye vyombo vya habari.

“taarifa binafsi ni muhimu kwa sababu inahusisha haki ya kila mtu kudhibiti taarifa zake. Tukishindwa kuelewa dhana hii vizuri, tunaweza kujikuta katika migogoro ya kisheria, kama ilivyotokea katika baadhi ya nchi ambapo kampuni kubwa zilipata hasara kwa kushindwa kuheshimu sheria za ulinzi wa taarifa binafsi,” amesema Dkt. Mkilia.

Aidha ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wahariri kuelewa misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi, wajibu wa Tume, pamoja na nafasi ya vyombo vya habari katika kulinda faragha za watu.

“Tumesisitiza umuhimu wa maadili ya uandishi wa habari, ili kuhakikisha kuwa taarifa binafsi za watu hazichapishwi hadharani bila idhini yao au uhalali wa kisheria, kwa kuzingatia sheria zinazosimamia sekta ya habari na mawasiliano,” alieleza Dkt. Mkilia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Bw. Deodatus Balile, amesema kuwa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi inapaswa kutazamwa kwa umakini ili isiwe chanzo cha mkanganyiko katika jamii.

Naye Mhariri Mkuu wa Gazeti la Pambazuko, Bw. Simon Mkina, alionya juu ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, ambapo watu wengi sasa wanapiga picha au kuchukua taarifa za watu binafsi na kuzisambaza bila idhini yao.

“Kwa sasa, kila mwenye simu anaweza kupiga picha na kusambaza mtandaoni bila kujali athari zake kwa faragha ya mtu husika. Tatizo kubwa ni kwamba watu hawa si waandishi wa habari, lakini wanatumia vifaa vyao bila kufuata misingi ya uandishi wa habari. Hili ni jambo baya na halifai katika jamii inayoheshimu utu wa mtu,” alisema Mkina.

Aliwataka Watanzania kuacha tabia ya kupiga picha au kusambaza taarifa za watu bila ridhaa yao, kwani kufanya hivyo ni kuwadhalilisha na kuwanyima staha. Aliongeza kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kinapaswa kukemewa vikali.

Mwisho.