Home BUSINESS USAFIRI WA UMEME WAANZA KUPAA KATIKA SEKTA YA USAFIRI WA MTANDAONI TANZANIA

USAFIRI WA UMEME WAANZA KUPAA KATIKA SEKTA YA USAFIRI WA MTANDAONI TANZANIA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Pikipiki na bajaji zimeendelea kuwa uti wa mgongo wa mifumo ya usafiri katika mataifa mengi ya Afrika Mashariki, zikihudumu kama teksi, vyombo vya usafirishaji wa mizigo, na usafiri wa watu binafsi.

Sasa, mabadiliko kuelekea pikipiki na bajaji zinazo endeshwa kwa betri za umeme yamekuwa yakitarajiwa kwa hamu na wakazi wa miji mbalimbali nchini Tanzania.

Katika miezi ya hivi karibuni, Bolt Tanzania iliingia katika ushirikiano na Green Wheels Tanzania kuanzisha matumizi ya pikipiki za umeme (EV bikes) katika sekta ya usafiri wa mtandaoni, hatua inayotafsiriwa kama mageuzi makubwa kuelekea usafiri endelevu.

Mpango huu umelenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na kuongeza chaguo la usafiri linaloendana na mahitaji ya jamii ya kimataifa na watalii katika miji ya Tanzania. Muhimu zaidi, mpango huu unapunguza gharama za uendeshaji kwa madereva na kuongeza kipato chao.

Kwa kuzingatia kupanda kwa bei ya mafuta, pikipiki za umeme zinatoa mbadala wa gharama nafuu, hivyo kusaidia madereva wa usafiri wa mtandaoni kuboresha hali yao ya kifedha.

Kwa biashara nyingine, matumizi ya usafiri wa umeme yanaendana na malengo ya uendelevu wa kampuni, huku Bolt ikiwa kinara wa sekta ya usafiri wa mtandaoni nchini, ikitoa mfano kwa washindani wake na kuhimiza matumizi ya teknolojia ya magari ya umeme ambayo tayari imepata mafanikio makubwa katika mataifa ya Magharibi.

Mbali na faida za kiuchumi, Green Wheels Tanzania inahakikisha kuwa mpito huu unachangia malengo ya Tanzania ya utunzaji wa mazingira.

“Pikipiki zetu za umeme hupunguza takriban 8.3KG ya uchafuzi wa CO2e kwa kila kilomita 100 ikilinganishwa na pikipiki za petroli. Kati ya pikipiki milioni 1.4 zilizosajiliwa nchini, nyingi huchangia uchafuzi mkubwa wa mazingira kupitia uzalishaji wa gesi na chembe hatarishi,” inasema taarifa ya Green Wheels Tanzania kwenye tovuti yake greenwheels.tz.

Akizungumzia ushirikiano huu, Dimmy Kanyankole, Meneja Mkuu wa Bolt Tanzania na Kenya, alisema: “Ushirikiano huu ni hatua thabiti ya kubadilisha mfumo wa usafiri wa mtandaoni.

Kwa kuanzisha pikipiki za umeme Arusha, tunarahisisha gharama kwa madereva na kuboresha uzoefu wa usafiri kwa abiria.”

Ingawa wananchi wameanza kukumbatia usafiri wa umeme katika maisha yao ya kila siku, changamoto kama kodi kubwa za uagizaji, utaratibu usio wazi wa usajili, na ukosefu wa fursa za ufadhili bado zinakwamisha ukuaji wa sekta hii. Kwa mujibu wa Ripoti ya E-Mobility Alliance ya 2024, masuala haya yanapaswa kushughulikiwa ili kuruhusu maendeleo ya haraka ya teknolojia ya EV nchini Tanzania.

Licha ya changamoto hizi, Tanzania inabakia miongoni mwa mataifa yanayoongoza Afrika katika mageuzi ya usafiri wa umeme, ikiwa na zaidi ya magari 5,000 ya umeme yakifanya kazi nchini.