Home BUSINESS TPA YANG’ARA UTENDAJI BORA

TPA YANG’ARA UTENDAJI BORA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepokea pongezi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa utendaji wake kwa mwaka 2023/24.

Ripoti ya CAG, iliyowasilishwa jana kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ilionesha kuwa TPA ni miongoni mwa mashirika ya umma yaliyozidi kufanya vizuri, ikiwa ni miongoni mwa mashirika yaliyopata asilimia 99.5 ya hati za ukaguzi (maoni) zilizotolewa kwa mashirika kuwa safi na za kuridhisha.

Katika uwasilishaji wake kwa Rais, CAG Charles Kichere alisema utendaji wa TPA ni mfano mzuri wa jinsi mashirika ya umma yanavyostawi kwa usimamizi mzuri kifedha.

“Ningependa kutambua mchango wa Serikali, uliosaidia mashirika 31 ya umma kufanya vizuri na kupata faida mwaka 2023/24,” alisema Kichere.

Miongoni mwa mashirika hayo ni TPA, iliyoripoti faida ya Sh bilioni 140.48. Mbali na TPA, mashirika mengine yaliyopata faida ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), lililopata faida ya Sh bilioni 248.75, na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Sh bilioni 242.9.

Ripoti ilionesha kuboreka utendaji wa mashirika ya umma, ambapo hati za ukaguzi 1,295 ( 99.5%) zilikuwa za kuridhisha, tano ( 0.4%) za shaka, na moja ( 0.1%) iliyokosa kutolewa maoni.

Kwa TPA, matokeo mazuri yaliyochangia faida, yanatokana na maboresho yaliyofanywa chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu wake, Plasduce Mbossa.

Maboresho hayo, ni pamoja na kuongeza ufanisi katika bandari kuu ya Dar es Salaam, ambapo ujio wa wawekezaji Dubai Port World (DP World) umeongeza ufanisi wake.

Uwekezaji katika vitendea kazi, rasilimali watu na mchakato wa kuboresha upakiaji na ushushaji mizigo, umepunguza kwa kiasi kikubwa muda wa meli kukaa bandarini.

Mafanikio mengine yalitokana na maboresho na ujenzi wa bandari mpya ya Mbamba Bay ya Ziwa Nyasa.

Hivi karibuni, Kamati ya Miundombinu ya Bunge ilitembelea bandari ya Dar es Salaam na kuipongeza kwa utendaji mzuri wenye tija kwa Taifa.

Akijibu ripoti ya CAG, Rais Samia alisema Serikali itatekeleza mapendekezo ya ripoti za CAG na Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwenye mashirika ya umma.

Rais Samia alisema Serikali itafanyia uchambuzi wa kina matokeo ya ripoti na kuchukua hatua stahiki, kuboresha utawala bora.

“Tutasikiliza kwa umakini mijadala ya Bunge kuhusu ripoti ya CAG, na kwa ripoti ya TAKUKURU, tutachukua hatua kwa mapendekezo yote ili kuimarisha utawala bora nchini,” alisema.

Rais Samia alishukuru ofisi ya CAG kwa kufanya ukaguzi wa kina, akisema matokeo ya ukaguzi yanathibitisha mafanikio ya juhudi za Serikali kuboresha ufanisi wa mashirika ya umma na kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali za umma.

“Licha ya changamoto zilizotajwa, kuna ongezeko la ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za Serikali, ambalo ni ishara nzuri ya maendeleo ya uwazi na uwajibikaji,” aliongeza Rais.

Hata hivyo, si mashirika yote ya umma yalipata hati safi. Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) liliripoti hasara ya Sh bilioni 27.78 mwaka 2023/24, likiwa ni ongezeko kubwa kutoka hasara ya Sh bilioni 4.3 mwaka uliopita.

Vilevile, Shirika la Reli la Tanzania (TRC) , ni miongoni mwao, likiripoti hasara ya Sh bilioni 224.

Licha ya changamoto hizo, Rais Samia alikiri kuwa baadhi ya masuala yaliyoibuliwa katika ripoti, yanatokana na matatizo ya muda mrefu, akikiri kuwapo juhudi za Serikali kuboresha usimamizi wa kifedha na kukuza mifumo ya uwazi katika mashirika ya umma.

MWISHO.