Home BUSINESS TGDC YATOA ELIMU KWA WANAVIJIJI WANAOZUNGUKA JOTOARDHI

TGDC YATOA ELIMU KWA WANAVIJIJI WANAOZUNGUKA JOTOARDHI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) imetoa elimu na uhamasishaji kwa wananchi wa vijiji vya Nsongwi Juu, Nsenga na Mbeye I, ili kuimarisha uhusiano na jamii zinazozunguka miradi ya jotoardhi ngozi.

Ziara hiyo ilifanyika Machi 17 hadi 20, mwaka huu na wakazi wa maeneo hayo kunufaika na elimu iliyotolewa na kuonesha utayari wa kulinda miundombinu inayozunguka miradi hiyo.

Wataalamu wa TGDC, Khadija Ahmed, Mhandisi Luhinda Luyagwa, Mhandisi Esther Range, Juma Mpamba, Boaz Mazigo, Joshua Nelei, Omary Seleman na Leonce Komba, kwa nyakati tofauti walieleza wananchi umuhimu wa kutunza na kulinda miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Wawakilishi hao walitoa elimu ya ufahamu na umuhimu wa utunzaji mradi pindi shughuli za uchimbaji zitakapoanza, kwa ajili ya uhakiki wa rasilimali ya jotoardhi, ikiwa ni safari kuelekeza uzalishaji umeme utokanao na jotoardhi.

Walisisitiza umuhimu wa wananchi kuona miradi na miundombinu yote iliyowekwa na itakayowekwa kama miradi yao, wakiilinda kwa kuwa inatekelezwa na Serikali.

“Miradi hii itanufaisha wananchi wote, hivyo tunaomba muitunze na kuilinda, kwani ni yenu,” alisema Khadija.

Pamoja na mengine, waliahidiwa kuwa sehemu ya watekeleza mradi kupitia ajira kwa kuzingatia wazawa wakiwamo vibarua, walinzi na nyingine.

Aidha, maofisa hao wa TGDC waliomba wananchi kutunza mazingira kwani ni moja ya kampeni zao na hata umeme wa jotoardhi utakapozalishwa, hautachafua mazingira bali utakuwa rafiki wa mazingira.

Waliombwa kuwa na mawasiliano, ili inapotokea changamoto basi iwe rahisi kutatuliwa.

Wananchi wa Nsongwi Juu, walishukuru TGDC kwa elimu iliyotolewa na walihitaji na ufafanuzi wa jinsi wazee wenyeji waliotunza mazingira watakavyonufaika na mradi, utoaji vipaumbele vya ajira kwa wazawa na uboreshaji miundombinu ya barabara, mambo yaliyotolewa ufafanuzi kwa kuhakikishiwa ajira na uboreshaji wa barabara.

Wanakijiji cha Nsenga waliuliza namna ya kunufaika na mradi ikiwamo ajira kwa vijana na miundombinu ya barabara, jambo lililotolewa ufafanuzi na kuhakikishiwa ajira za muda wakati wa utafiti na za kudumu, wakati wa uzalishaji, uboreshaji miundombinu na ushirikiano baina ya TGDC na wananchi.

Wanakijiji cha Mbeye I, waliishukuru TGDC kwa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono shughuli za jamii ya wana Mbeye I, ikiwamo kupeleka maji katika shule ya msingi Mbeye I, jambo lililowapunguzia ajali wanafunzi waliokuwa wakivuka barabara kufuata maji.

Pia ugawaji mikoba kwa wanafunzi wa shule hiyo na vifaa kama madaftari.

Katika hatua nyingine, wana Mbeye I walilaani uharibifu wa miundombinu unaofanywa na watu wasio waaminifu na kuahidi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa kuilinda, huku wakiiomba TGDC kuendelea kuishika mkono kwenye ujenzi wa zahanati na madarasa ya shule na barabara. 

TGDC iko mbioni kuhakiki rasilimali ya jotoardhi katika miradi mitano ya kipaumbele ya Ngozi na Kiejo-Mbaka (Mbeya), Songwe (Songwe), Luhoi (Pwani) na Natron (Arusha) ili kuzalisha megawati 200 za umeme mwaka 2030. 

Kwa sasa itaanza na mradi wa jotoradhi Ngozi (70Mw) na baada ya uhakiki, hatua ya uzalishaji itafuata.

Mwisho.