


Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es salaam, Geofrey Mkinga wakati wa semina ya siku moja kwa wahariri wa vyombo vya habari iliyoandaliwa na wakala huyo.
Mkinga amesema mafanikio hayo ya TARURA yanatokana na ongezeko kubwa la bajeti ya Wakala kutoka Sh. Bilioni 275 hadi Sh. Bilioni 870.3 sawa na ongezeko la asilimia 216 kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2024/25.
“Mtandao wa barabara za lami katika kipindi hicho umeongezeka pia kutoka Km. 2,025.69 hadi Km. 3,337.66, na changarawe kutoka Km. 27,809.26 hadi Km. 42,059.17 na barabara za udongo zimepungua kutoka Km. 112,317.20 hadi Km. 99,032.93. Madaraja yaliyojengwa yamefikia 3,195 na makalavati 75,620,” amesema
Aidha Mkinga amesema katika ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na Wakala wanaendelea kufanya majaribio kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ya mawe na madaraja ya mawe pamoja na teknolojia nyingine katika kuboresha barabara tunazozisimamia.
Amesema matumizi ya teknolojia na malighafi za ujenzi zinazopatikana eneo la kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya barabara, huongeza ufanisi, huokoa muda, hutunza mazingira kwa gharama nafuu.
“Matumizi ya teknolojia mbadala na malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi kwaajili ya ujenzi wa barabara na madaraja imeweza kupunguza gharama zaidi ya asilimia 50 ambapo TARURA imeweka kipaumbele cha kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi,” amesema
Amesema jumla ya madaraja ya mawe 350 yamejengwa ambapo gharama zimepungua kwa kiasi cha Sh.Bilioni 10. Kwa upande wa majaribio ya teknolojia mbadala Km. 7.95 zimekamilika na Km. 53.76 zipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na ufuatiliaji wa ubora wa teknolojia hizo unaendelea.
“Haya yote ni matokeo ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mtandao wa barabara za wilaya, kwa kuwa maeneo ya kilimo vijijini yakiwa yanafikika kwa mwaka mzima, inaongeza ukuaji wa kilimo na kupunguza umaskini,” amesema
Hata hivyo amesema Wakala unaendelea na matumizi ya malighafi za ujenzi wa barabara zinazopatikana maeneo ya kazi na utafiti wa teknolojia mbadala za ECOROADS, Ecozyme, na GeoPolymer kwenye ujenzi wa barabara kwa lengo la kupata ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kulinda mazingira.



Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameziomba taasisi za serikali ikiwemo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) na Tarura ziweze kusomana na kuwasiliana katika utendaji kazi ili kuondoa hasara zinazoweza kutokea wakati wa utekeleaji wa majukumu yao.
“Nalisema hili kwa sababu niwahi kushuhudia eneo moja barabara imejengwa vizuri na kukamilika lakini wakaja Dawasa kubomoa na kupitisha mabomba ya maji wanaacha Barabara inaharibika, sasa nikajiuliza kama mifumo yao ingesomana haya yote yasingetokea kwani tayari gharama zimetumika kisha watu wanabomoa na kusababisha hasara,” amesema Balile
Aidha Balile ameiomba Tarura kushirikisha waandishi wa Habari wakati wakifanya kampeni mbalimbali hasa za kuwataka watu kuacha kuharibu miundombinu ya barabara na ya kuwaondoa wafanyabiashara katika hifadhi za barabara.




