DAR ES SALAAM
Mwimbaji nguli wa Muziki wa Injili Afrika Mashariki na Kati, Rose Mhando amesema amekiri kwamba Mkurugenzi wa Msama Promotions ambaye ni mwandaaji wa matamasha mbalimbali ya Muziki wa Injili Alex Msama, ni zaidi ya Baba kwake kwani tangu alipoanza kazi zake za Uimbaji wa nyimbo za Injili amekuwa akifanya naye kazi kwa wema bila dhuluma nakwamba Msama hajawahi kumdhulumu.
Muhando alisema yeye pamoja na baadhi ya wasanii wenzake wa muziki wa Injili, hawawezi kujivunia mafanikio yao bila kutaja jina la Alex Msama ambaye hivi karibuni alipata tuzo ya Muandaaji Bora wa Muziki wa Injili wa wakati wote
Rose ametoa kauli hiyo baada ya hivi karibuni kuwapo taarifa kwenye mitandao ya kijamii, zikidai msanii huyo aliwahi kudhulumiwa haki zake na Msama.
Akizungumzia kuhusu madai hayo, Rose alisema ameshitushwa na kusikitishwa sana na tarifa hizo, na kuongeza kuwa hajui zimetokea wapi na watunzi wa uzushi huo wana lengo gani.
Alisema katika maisha yake mafanikio yake ya muziki, hawezi kumsahau wala kutaja jina la Msama ambaye ametumia muda mwingi wa maisha yake na fedha zake kuibua, kukuza na kulea vipaji wa vya muziki wa Injili na kuhakikisha haki zao zinalindwa.
Akitolea mfano, Rose anasema “Msama alikuwa ananisaidia kutoa ushauri wakati wa kuandaa muziki, alitoa msaada mkubwa wa fedha kuingia studio na kurekodi, zaidi ya yote alianzisha vita ya kukabiliana na wahuni waliokuwa wakiiba na kuuza ‘CD’ zetu na kuwafanya wasanii kukosa haki zao na kuishi maisha ya shida.
“Kwangu mimi, Msama ni zaidi ya Baba, amenisaidia mambo mengi sana, kuanzia fedha hadi ushauri, amenivumilia hata ninapomkwaza. Leo mtu anaweza kuchapisha taarifa na kueleza kwamba eti Msama aliwahi kunidhulumu, hii sio kweli kabisa sijawahi na siwezi kusema kauli hiyo dhidi ya Msama” alisisitiza Rose Muhando.
Alisema kuwa “yapo mambo madogo ya kibinadamu yaliyowahi kutokea wakati wa kazi, ikiwamo mimi mwenyewe kumkwaza Msama, lakini hiyo haina maana kwamba Msama amewahi kunidhulumu haki zangu
Aliongeza kuwa ataendelea kufanya kazi na Msama wakati wowote atakapohitajika na ataendelea kuwa chini yake kwani anaamini mfanyabiashara huyo ana mapezi ya dhati ya muziki wa Injili toka moyoni na Serikali inapaswa kumuangalia kwa jicho tofauti na hata kumpa msaada.
“Mimi na baadhi ya wasanii wenzangu tulifika hatua ya kumuita Msama kuwa ni Askofu wa Muziki wa Injili, yule Baba ana mapenzi na muziki wa Injili toka moyoni, ni mtumishi wa Mungu aliyeamua kufanya utumishi wake kwa kukuza vipaji vya wasanii wa muziki huo” aliongeza.
Amemuomba Mh Rais D kt.Samia Suluhu Hassan kumuangalia Msama na kumlinda pale anaponyanyaswa na baadhi ya watendaji wa Serikali kwani kumuua Msama ni kuuwa ndoto na maisha ya wasanii wa Muziki wa Injili.
Kuhusu hatma yake kwenye muziki huo, Rose alisema muda mrefu alijiweka kando kutokana na changamoto za kiafya, lakini hivi sasa anaandaa Albamu mpya ya muziki wake ambayo itazinduliwa wakati wowote mwaka huu.
“Baada ya kutoka hospitali, nilijipa muda wa kupumzika, lakini hivi sasa naandaa Albamu yangu ya kukata na shoka, itazinduliwa wakati wowote mwaka huu na itakapokuwa tayari nitawajulisha washabiki wangu,”