Home BUSINESS MAFANIKIO YA NHC MIAKA MINNE YA UONGOZI WA Dkt. SAMIA MADARAKANI

MAFANIKIO YA NHC MIAKA MINNE YA UONGOZI WA Dkt. SAMIA MADARAKANI

– Thamani ya Shirika yaongezeka, yafikia Sh. trilioni 5.47
– Mapato yapaa mara dufu hadi Sh. bilioni 9.4 
– Miradi ya Shirika yatekelezwa kwa asilimia 100

Na; Mwandishi Wetu.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, amekuwa chachu ya mageuzi makubwa katika sekta ya nyumba nchini katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.

Mageuzi haya katika sekta ya nyumba nchini Tanzania yanachagizwa na uwepo wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),kutokana na ukweli usiopingika kwamba NHC ndiyo chachu ya mageuzi haya makubwa.

Niwazi kwamba NHC tangu kuundwa kwake muda mfupi baada ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka 1961 ni kuwawezesha Watanzania kupata makazi bora.

Shirika hili lilianzishwa mwaka 1962 chini ya Sheria ya Bunge Na. 45 na tangu wakati huo, limekuwa likitimiza jukumu lake hilo la kipekee kwa Watanzania kuwapatia makazi bora.Hayo ndio maono ya NHC, iliyoyaakisi kutoka kwa muasisi wake, Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, yaliyoendelezwa na viongozi wa awamu zilizofuata na sasa taifa likiwa katika Awamu ya Sita ya uongozi, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, anayetimiza miaka minne madarakani Machi 19, mwaka huu 2025.

Hakuna wa kubisha kwamba utendaji wa NHC unaongozwa na Dira ya Maendeleo Endelevu ya Makazi, ambayo imepata msukumo na kasi mpya, zilizozaa mafanikio makubwa ya kupigiwa mfano, yaliyoacha historia ya kipekee kwa Watanzania ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Safari ya mafanikio NHC 

NHC ambayo hadi sasa imeshaongozwa na wakurugenzi tofauti 12 tangu kuanzishwa kwake, awali ilitekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya umma, ikiwamo kuwajengea na kuwauzia wananchi kwa gharama nafuu. Hata hivyo, baadaye kuliibuka changamoto za kiuchumi na kisheria, ambazo ziliathiri utendaji wa NHC, lakini zilitafutiwa ufumbuzi.Ufumbuzi huo ni pamoja na kufanyika kwa mageuzi yanayotajwa kuwa ya kihistoria hadi mwaka 2008. Wakati huo kulitokea mabadiliko ya kuziondoa sheria zisizo rafiki katika maendeleo ya sekta ya nyumba.

Ndipo Shirika la Nyumba la Taifa, lilipewa mamlaka mapya ya kujiendesha kibiashara, lakini bila kusahau jukumu lake la msingi. Hatua hizi ziliweka msingi wa kuboresha huduma za makazi kwa Watanzania. Hata hivyo, katika kipindi cha uongozi wa Rais Dk. Samia, kasi ya utekelezaji wa miradi ya nyumba imeongezeka kwa kiwango cha kipekee.

Ukuaji Mapato NHC

Sera imara za Serikali ya Awamu ya Sita, zimewezesha ukuaji wa NHC, ambapo sasa ankara za kodi ya nyumba zimepanda kutoka shilingi 7.5 bilioni mwaka 2021 hadi kufikia shilingi 9.4 bilioni. Makusanyo ya kodi hiyo yamefikia zaidi ya asilimia 100.

Mwaka 2021, NHC lilikuwa na maeneo yasiyopangishwa yanayofikia nyumba 700, lakini sasa maeneo hayo yameshapangishwa kwa asilimia 80. Hii ni kutokana na kuimarika kwa uchumi na biashara za Watanzania.

Upande wa madeni, NHC imefanikiwa kukusanya madeni yake, ambapo katika kipindi miaka minne zimekusanywa Shillingi 8.3 bilioni.

Mbali na hayo, NHC pia imeongeza mauzo ya nyumba mpya, huku takwimu zikionyesha katika Mradi wa Kawe pekee nyumba zote 560 zimeshauzwa kabla mradi kukamilika.

Hali hiyo inatajwa kutokana na kipato cha wananchi kuimarika wakiwemo wapangaji wa nyumba na majengo ya NHC kote nchini.

Thamani rasilimali NHC yaimarika

Hadi kufikia Juni 2024 kwa hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), thamani ya rasilimali za NHC imeimarika na kufikia Shilingi 5.47 trilioni, ikilinganishwa na mwaka 2021 ambao zilikuwa Shilingi 5.04 trillioni.

Ukuaji huo unaelezwa ni kutokana na kuongezeka kwa milki za Shirika ukichagiwa na kukamilika nyumba mpya na umiliki wa maeneo mbalimbali, ikiwemo NHC kufanikiwa kununua ardhi na majengo katika eneo la Urafiki, Dar es Salaam, yaliyokuwa yakimilikiwa awali na Kampuni ya Tanzania-China Friendship Textile Mills Co (Urafiki).

Ushirikiano na Sekta ya Fedha 

Kupitia ushirikiano na benki zaidi ya 22, NHC limewezesha wananchi kupata mikopo ya nyumba ya muda mrefu. Sera ya ubia iliyohuishwa mwaka 2022 pia imefungua milango kwa sekta binafsi kushiriki katika miradi ya nyumba yenye thamani ya Shilingi 191 bilioni. 

Miradi Awamu ya Sita

Katika kipindi hicho cha Awamu ya Sita madarakani, NHC imekamilisha miradi mikubwa ya nyumba za makazi. Miradi hiyo ni pamoja na; Mradi wa vyumba 887 za makazi katika eneo la Iyumbu na Chamwino, mkoani Dodoma.

Miradi hiyo imejengwa eneo la Iyumbu (303) na Chamwino (101) Jijini Dodoma, nyumba nyingine mpya 68 ujenzi unaendelea eneo la Iyumbu uliofikia asilimia 90; Pia kuna  na ujenzi wa nyumba 521 za makazi na biashara katika maeneo ya Dar es Salaam; Medeli Dodoma na Mtukula-Kagera.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika hilo, tangu lilipoanzishwa hadi sasa, limefanikiwa kujenga nyumba 30,000 za makazi, huku likiendelea kujenga nyumba za kuuza nyumba na kupangishwa.

Ikumbukwe kuwa katika Mwaka 2015, NHC lilianzisha Mpango Mkakati wa Miaka 10 (2015/16 – 2024/25), uliolenga kujenga nyumba 10,000 na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi. Katika kipindi cha Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, NHC imekamilisha miradi mikubwa ya nyumba za makazi.

Miradi miwili mikubwa Awamu ya Sita

Ndani ya kipindi hicho, NHC lilipanga kukamilisha miradi mikubwa ambayo ilisimama tangu mwaka 2018, ambapo Rais Dk. Samia alipoingia madarakani, aliinusuru hivyo pia kuliruhusu Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuliwezesha kukopa fedha za kuikamilisha miradi hiyo ya kimkakati.

Kawe 711

Sehemu ya majengo Mradi wa Kawe unaoendelea kujengwa 

Januari mwaka 2024, Mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Estim Construction Company Limited ilirejea kazini na ujenzi wa mradi wa nyumba 422 pamoja na sehemu za biashara sasa unaendelea katika mradi wa Kawe 711, wenye thamani ya Shilingi 169 bilioni, ambao sasa ujenzi wake umefikia asilimia 50, ukitarajiwa kukamilika Aprili 2026.

‘Samia Housing Scheme’

Sehemu ya Mradi wa Samia Housing Scheme

Katika kutambua mchango wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuendeleza sekta ya nyumba tangu alipoingia madarakani, NHC ilibuni mradi wa nyumba 5,000 uliopewa jina la Samia Housing Scheme, ulioleta matumaini mapya kwa wananchi. 

Mradi huo unatekelezwa eneo la Kawe, Dar es Salaam, ambapo ujenzi wa nyumba 560 ulikwishaanza ukifikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika Februari mwaka huu 2025.

Samia Housing Scheme utawezesha ujenzi wa nyumba 5,000 katika maeneo mbalimbali nchini zote zikigharimu Shilingi 466 bilioni.

Tayari NHC imekamilisha mauzo ya nyumba 560 eneo la Kawe huku shirika hilo likijiandaa kuanza awamu ya pili ya mradi huo na Medeli Dodoma  (100).

Morocco Square

Jengo la Morocco Square linavyoonekana 

Miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Shirika la Nyumba la Taifa pia limefanikiwa kukamilisha mradi wa Morocco Square kwa asilimia 100.

NHC inaendelea kuuza na kupangisha, ambapo maeneo ya maduka (Retail Mall) yamepangishwa kwa asilimia 100 huku asilimia 95 ya Ofisi zikipangishwa pia.

Kwenye jengo lenye nyumba za makazi 100, eneo hilo tayari nyumba 85 zimeuzwa, huku mauzo ya nyumba zilizobakia yakiendelea na upangishaji wa hoteli yenye vyumba 81 umefanyika kwa asilimia 100 na hoteli hiyo ikiwa tayari imeanza kutoa huduma.

Kimsingi miradi ya Kawe 711 na Morocco Square inaenda kuboresha mandhari ya Jiji la Dar es Salaam, kuboresha na kukuza uchumi wa Tanzania.

Majengo ya kimkakati, ofisi na biashara 

2H Commercial Building – Morogoro – Ujenzi wa jengo hili la biashara umefikia asilimia 40.

Masasi Plaza – Masasi Mtwara – Ujenzi wa jengo la biashara katika mji wa Masasi upo asilimia 40.

Kahama – Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Januari 2025.

Mradi wa ujenzi unaoendelea Kahama

Mtanda Lindi- Ujenzi wa jengo la biashara Mtanda Commercial Building-Lindi umefikia asilimia 30.

Mradi  unaoendelea Lindi

 

Usimamizi miradi na usanifu

Miaka minne ya utawala wa Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inashuhudia NHC likiwa msimamizi na mshauri elekezi wa miradi mbalimbali nchini. 

Miradi hiyo ni pamoja na usimamizi wa ujenzi Soko Kuu la Kariakoo ulio na thamani ya Shilingi bilioni 28 na ambao umeshakamilika kwa wastani wa asilimia 97. Mradi huu ulitarajiwa kukamilika Januari 2025.

Mradi wa pili unaosimamiwa na NHC ni usanifu na usimamizi wa jengo la Ofisi ya Wizara ya Fedha na Mipango eneo la Mtumba umekamilika na ujenzi umefikia asilimia 85, mjenzi akiwa ni Kampuni ya Estim Construction.

NHC pia inasimamia wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, awamu ya pili ujenzi umefikia asilimia 88, huku mjenzi akiwa ni Suma JKT;

Mradi wa nne ambao pia unasimamiwa na NHC ni usanifu na ujenzi wa jengo la Soko la Madini (Tanzanite) eneo la Mirerani Manyara.Tayari usanifu umekamilika na ujenzi umefikia asilimia 86.

Sera ya Ubia

Baada ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, alifungua milango ya uwekezaji nchini na kuhimiza ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma lengo likiwa kuharakisha ujenzi wa uchumi wa Tanzania.

Katika kuenda sanjari na maono ya Rais, NHC liliboresha sera yake ya ubia, ambayo ilizinduliwa Waziri Mkuu Novemba 16, 2022.

Mwaka 2024, NHC liliidhinisha na kusaini mikataba ya miradi 21 ya ubia iliyo na thamani ya Shilingi 179 bilioni.

Mojawapo ya miradi ya ubia unaoendelea kujengwa eneo la Kariakoo

Tayari NHC imepata vibali kwa miradi 18 vya ujenzi na umeanza kutekelezwa ukifikia hatua mbalimbali, huku miradi mingine mitatu ikiwa imeshapata vibali hivi karibuni na itaanza kutekelezwa.

NHC inaendelea kusimamia miradi ya ubia mipya na ile ya zamani, ambayo awali ilisimama ikiwa maeneo mbalimbali nchini na tayari miradi minne iliyosimama awali imesharejeshwa NHC ili ikamilishwe. Shirika la Nyumba la Taifa linalenga kuhakikisha miradi yote ya ubia isiyokamilika inarejeshwa na mazungumzo na wabia wenye miradi hiyo yanaendelea.

NHC inaendelea na upembuzi, pia tathimini ya kina kwa waombaji wapya kwa miradi katika maeneo kadhaa yanayohitaji kuendelezwa, ambapo sasa ipo kwenye hatua ya kupata idhini ya kuendeleza viwanja takriban 80 nchi nzima.

Shirika la Nyumba la Taifa limefanya mageuzi makubwa katika kushirikiana na sekta binafsi kujenga majengo ya kisasa ya makazi na biashara likipendezesha mandhari ya miji yetu. Mfano, eneo la Kariakoo lililokuwa na wapangaji 172, ambao nyumba zao zimevunjwa na kuendelezwa, sasa lina zaidi ya nyumba 2,100 za makazi na biashara.

Miradi ya ukandarasi

Kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kimeshuhudia NHC ikipewa miradi mbalimbali ya kimkakati ya ukandarasi, iliyo na thamani ya Shilingi 186 bilioni iliyokamilika au ipo hatua za mwisho za utekelezaji, eneo la Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma ikiwamo ujenzi wa majengo ya Ofisi Nane za Wizara uliofikia asilimia 90.

Sehemu ya majengo ya Mradi wa Ofisi Nane za Serikali unaotekelezwa na NHC, Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma.

NHC imetekeleza miradi mingine katika Awamu ya Sita ikiwemo ujenzi wa Jengo la Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, uliofikia asilimia 80 kwa gharama ya Shilingi 9.7 bilioni.

Ujenzi wa jengo la ofisi pamoja na uzio wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Temeke Dar es Salaam ambao sasa umefikia asilimia 40 na ujenzi wa ghala la chakula la Halmashauri ya Masasi Vijijiniambao umemilika.Ujenzi wa Hospitali za Kanda ya Kusini (Mitengo) na Hospitali ya Kanda ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Musoma, Mara uliokwishakamilika pamoja na ukamilishaji wa Jengo la Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete ambayo nayo imekamilika kwa asilimia 100.

Shirika pia limejenga majengo mawili ikiwemo ofisi na miundombinu kwa ajili ya tanuru (incinerator) la Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekamilika jijini Dodoma, pia linajenga jengo la Tanzanite Mererani, Mkoa wa Manyara ambao upo asilimia 86.

Katika kipindi hicho, NHC inakamilisha pia ujenzi wa miradi 17 yenye majengo 44 ya Wakala wa Misitu Tanzania-TFS kwa thamani ya Shilingi 12.96 bilioni huku pia likitekeleza ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dodoma uliofikia asilimia 34.

Matengenezo 

NHC inakamilisha ukarabati wa majengo katika mikoa mbalimbali ya shirika, unaojumuisha ujenzi wa mifumo ya maji takana kupaka rangi.  Tangu mwaka 2023 bajeti ya Shilingi 7 bilioni imekuwa ikitengwa kila mwaka kwa ajili ya ukarabati wa nyumba zake pote nchini, hali inayoelezwa kuwezekana kwa kilichotajwa ni kuimarika kwa uwekezaji na mapato ya Shirikala Nyumba la Taifa.

Miradi inayoanza  

Miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa kwa mafanikio makubwa. Ndani ya NHC kwa sasa kuna miradi inayokaribia kuanza, ukiwamo wa Samia Housing Scheme Kawe Awamu ya 2 na Kijichi Jijini Dar es Salaam, Singida 2F mkoani Singida, Kashozi Business Center, Bukoba Mjini huku miradi mingine ikiwa ni Mt. Meru Plaza eneo la Kibla jijini Arusha, Mkwakwani Plaza Tanga, Juwata Plaza Morogoro, Medeli Awamu ya 3 Dodoma na Tabora Commercial complex.

Miradi mingine ni Mpwapwa Flats Dodoma, Ilala Breweries Retail Shops, Iringa ICC na Mtwara Warehouse.

Mustakabali wa NHC

NHC linaendelea kupanua wigo wa shughuli zake kwa kutumia teknolojia za kisasa na utaalamu wa ndani huku miaka ijayolikitarajia kuendelea kuanzisha miradi mipya ya makazi, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, bila kuliacha kando Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), ujenzi wa vitega Uchumi, kutekeleza miradi ya ukandarasi na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa miradi mbalimbali nchini pamoja na kutekeleza sera ya ubia.

Tunaweza kusema kwamba miaka minne ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan, Shirika la Nyumba la Taifa, limepiga hatua kubwa katika kuboresha makazi na sekta ya nyumba nchini. Hatua hiyo inadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha kila mmoja anapata haki ya makazi bora. Kwa mipango madhubuti, NHC itaendelea kuwa mwanga wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.