Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono waandamanaji kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 08 Machi, 2025.




Arusha, 08 Machi – 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ina dhamira ya kujenga Tanzania jumuishi, yenye ustawi na haki na kupinga ubaguzi kwa sababu zozote zile, ziwe za kidini, kikanda, kiitikadi au jinsia.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati wa kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewaelezea wananchi hatua kubwa ambazo Tanzania imepiga katika kufikia malengo ya Azimio la Ulingo wa Beijing wa mwaka 1995 na yale malengo 17 ya Dira ya Maendeleo Endelevu.
Rais Dkt. Samia amesema Serikali inaendelea na itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kisheria katika kupambana na mila kandamizi na ubaguzi kwa mwanamke na mtoto wa kike hivyo kuwezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa katika usawa wa kijinsia.
Vile vile, Rais Dkt. Samia amesema maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kuchukua hatua kuhakikisha kwamba kila msichana na mwanamke hapa nchini anapata nafasi sawa ya kufikia ndoto zake.
Akigusia mwelekeo wa harakati za usawa wa kijinsia katika kupata fursa na manufaa, Rais Dkt. Samia amesema kuwa uendelevu wa harakati hizo utategemea uwekezaji utakaofanywa kwa vijana ambao watakuwa kizazi kijacho cha wapambanaji.
Akiwapongeza maelfu ya wanawake walioshiriki maadhimisho hayo ikiwemo maandamano ya wanawake waliopo kwenye sekta mbalimbali za uchumi, Rais Dkt. Samia amesema kuwa jeshi la wanawake sio tu ni jeshi kubwa, bali ni jeshi madhubuti na la kutumainiwa.
Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa Wanawake wote kuuungana pamoja katika kuhakikisha kwamba mabadiliko wanayoyahitaji, yanapatikana.
Sharifa B. Nyanga
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu