Na; Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM.
Imeelezwa kuwa katika kipindicha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, sekta ya utalii imeimarika na kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa Biashara katika sekta hiyo.
Mafanikio hayo yamechagizwa na uwepo wa filamu ya ‘The Royal Tour’ iliyomuhusisha Rais Samia yenye lengo la kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii na uwekezaji, vinavyopatikana hapa nchini, ikiwemo uwekezaji wa hoteli za kitalii.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Serena Hotel Afrika Bw. Ashish Sharma, amesema Serikali imekuwa na nia ya dhati katika kuhakikisha Biashara ya utalii inaimarika baada ya kupita kwenye janga la ugonjwa wa Corona, nakwamba baada ya Filamu ya ‘Royal Tour’ Biashara imeimarika kwa kiasi kikubwa.
‘Utalii sio kuona wanyama tu, bali ni pamoja na utamaduni wetu, watalii wanapokuja wanahitaji kupokelewa vizuri, kulala mahali salama na kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria’ amesema Bw. Sharma.
Aidha, ameongeza kuwa kwa sasa wanaendelea kuimarisha huduma zao katika hoteli hiyo kwa kufanya ukarabati na kuweka vyumba vya kisasa, nakwamba nusu ya hoteli hiyo imefungwa kwaajili ya ukarabati huo, huku huduma zote muhimu zinaendelea kutolewa kama kawaida.
‘Mabadiliko haya yanakadiriwa kuwa wa mwaka mmoja. Uongozi wa hoteli unatarajia kuzindua vyumba vya kisasa na vyakuvutia huku tukiendelea kuhakikisha wageni wetu wanaendelea kufurahia huduma zetu bila usumbufu wowote’ ameongeza.