Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la World Vision Tanzania, Bi. Nesserian Mollel, wakisaini hati ya makubaliano jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya ushirikiano kwenye Mradi wa Maji katika Kijiji cha Kwedizinga, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga. Benki ya Absa imetoa mchango wa TZS milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa kisima katika kijiji hicho kitakachowanufaisha wakazi zaidi ya 3,000, ambapo watoto wanawakilisha 55% ya idadi ya wakazi wa kijiji hicho.
Absa Bank Tanzania imetangaza ushirikiano wa kimkakati na Shirika la World Vision Tanzania ili kuboresha upatikanaji wa maji safi, usafi wa mazingira na watu katika kijiji cha Kwedizinga, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga. Mpango huu unaonyesha dhamira ya Absa ya kuwawezesha jamii na kuwa chachu ya maendeleo chanya.
Kijiji cha Kwedizinga, ambacho kina vijiji vidogo saba na idadi ya watu takriban 4,000, kimekuwa kikikabiliwa na changamoto za kupata maji safi na salama. Hivi sasa, wakazi wanategemea mabwawa na mito ya msimu, hali inayosababisha ongezeko la magonjwa yanayotokana na maji na kuweka mzigo mkubwa kwa wanawake na watoto ambao mara nyingi husafiri zaidi ya kilomita 2 kila siku kutafuta maji.
Mradi huu unalenga kushughulikia changamoto hizi kupitia hatua kuu zifuatazo:
Uchunguzi wa Kihidrolojia na Uchimbaji wa Visima: Kufanya uchunguzi wa kina wa maji chini ya ardhi ili kubaini eneo linalofaa zaidi kwa ajili ya kisima chenye mavuno mengi, ikifuatiwa na uchimbaji hadi kina cha mita 180.
Mfumo wa Kusukuma Maji kwa Nguvu za Jua: Kufunga mfumo rafiki wa mazingira wa kusukuma maji kwa kutumia nishati ya jua ili kusafirisha maji kutoka kisimani hadi kwenye tanki la kuhifadhi lililoinuliwa.
Uhifadhi na Usambazaji wa Maji: Kujenga tanki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 50,000 na kuanzisha mtandao wa usambazaji maji wenye vituo vingi vya ukusanyaji, kuhakikisha kwamba vijiji vidogo vyote saba vinapata maji safi ndani ya mita 400, sambamba na viwango vya sera ya maji ya Tanzania.
Ushirikishwaji wa Jamii na Mafunzo: Kuunda na kutoa mafunzo kwa kamati ya watumiaji wa maji ili kusimamia mfumo wa usambazaji maji, kukuza mbinu endelevu, na kufanya uhamasishaji wa jamii kuhusu usafi wa mazingira na usafi binafsi.
Mpango huu unalingana na Malengo kadhaa ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, ikiwemo SDG 3 (Afya Bora na Ustawi), SDG 4 (Elimu Bora), na SDG 6 (Maji Safi na Usafi wa Mazingira). Pia unaunga mkono Awamu ya 3 ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji ya Tanzania (2022/2025), ambao unalenga kuwaunganisha mamilioni ya watu na vyanzo vipya na vilivyoboreshwa vya maji.
Absa Bank Tanzania imejitolea TZS 50,000,000 kuwezesha mradi huu, ikionyesha dhamira ya benki ya kuiwezesha Afrika ya Kesho, pamojaz, hatua moja baada ya nyingine.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Bw. Obedi Laiser, Mkurugenzi Mtendaji wa Absa Bank Tanzania, alisisitiza dhamira ya benki ya kuwa chachu ya maendeleo chanya katika jamii wanazofanya kazi: “Katika Absa, tunaamini kwamba kila story ina umuhimu. Ushirikiano huu ni ushahidi wa lengo letu la kuiwezesha Afrika ya Kesho, pamoja, hatua moja baada ya nyingine. Kwa kutoa upatikanaji endelevu wa maji safi katika kijiji cha Kwedizinga, hatuboreshi tu afya na usafi wa mazingira, bali pia tunashughulikia masuala ya utofauti na ujumuishaji, fursa za kielimu, na kuwezesha ukuaji wa kiuchumi.“
Bi. Nesserian Mollel, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa World Vision Tanzania, pia alitoa maoni kuhusu ushirikiano huo: “World Vision imejitolea kufanya kazi na jamii kuleta maendeleo. Ushirikiano huu na Absa Bank Tanzania unaonyesha dhamira yetu ya kukuza mabadiliko ya kibinadamu. Pamoja, tunahakikisha kwamba watoto na familia katika kijiji cha Kwedizinga wanapata moja ya mahitaji ya msingi ya maisha – maji safi.“
Mradi unatarajiwa kunufaisha moja kwa moja wakazi wote 3,890 wa kijiji cha Kwedizinga na kuwanufaisha kwa namna tofauti watu wengine 596 kutoka vijiji jirani, hatua muhimu kuelekea kuboresha afya, elimu, na matokeo ya kiuchumi katika eneo hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (wa tatu kushoto) akibadilishana hati ya makubaliano ya ushirikiano na Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la World Vision Tanzania, Bi. Nesserian Mollel, jijini Dar es Salaam leo, ambapo kupitia makubaliano hayo Benki ya Absa imetoa mchango wa TZS milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa kisima cha maji kitakachowanufaisha wakazi zaidi ya 3,000 wa Kijiji cha Kwedizinga, Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga ambapo watoto wanawakilisha 55% ya idadi ya wakazi wa kijiji hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (katikati), Mkurugenzi wa Wateja wa Makampuni wa Absa Tanzania, Bi. Nellyana Mmanyi na Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la World Vision Tanzania, Bi. Nesserian Mollel wakifurahi jijini Dar es Salaam leo, muda mfupi mara baada ya kusaini hati ya makubaliano, kwa ajili ya ushirikiano katika Mradi wa Maji kwenye Kijiji cha Kwedizinga, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.