
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakiwapungia Waislamu walioshiriki katika kilele cha Tuzo za 33 za Kimataifa za kuhifadhi Qurani Tukufu kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Februari 23, 2025. Kushoto ni Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzani, Dkt. Abubakar Zubeir Ally katika kilele cha Tuzo za 33 za Kimataifa za kuhifadhi Qurani Tukufu kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Februari 23, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozwa na Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir Ally ( wa tatu kulia) kwenda kwenye jukwaa la kutoa zawadi kwa washindi wa Tuzo za 33 za Kimataifa za kuhifadhi Qurani Tukufu kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Februari 23, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi, Nadhiru Omar Ishengoma ufunguo wa gari baada ya kujishindia gari katika kilele cha Tuzo za 33 za Kimataifa za kuhifadhi Qurani Tukufu y kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Februari 23, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Nadhiru Omar Ishingoma akionesha ufunguo wa gari aliokabidhiwa na Mgeni Rasmi Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa baada ya kujishindia gari hilo katika kilele cha Tuzo za 33 za Kimataifa za kuhifadhi Qurani Tukufu kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Februari 23, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kasssim Majaliwa akimkabidhi zawadi ya Dola za Marekani 6000, Mohammed Yacine kutoka Algeria (kushoto kwake ) ambaye alikuwa mshindi wa kwanza wa kilele cha Tuzo za 33 za Kimataifa za kuhifadhi Qurani Tukufu kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Februari 23, 2025. Kushoto ni Sheikh Mkuu na Mufti wa tanzania, Dkt Abubakar Zubeir Ally. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
DAR ES SALAAM
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa madhehebu ya dini kuendelea kufundisha na kuimarisha elimu ya dini ili kutoa fursa kwa watoto na vijana kupata elimu hiyo na kuwaandaa kuwa watu wema.
Ametoa wito huo leo Jumapili (Februari 23, 2025) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha Tuzo za 33 za Kimataifa za Kuhifadhi Qurani Tukufu. yanayofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Jukumu la kuhakikisha maadili bora ni la kwetu sote, madhehebu ya dini yakiwa na mchango mkubwa. ”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amehimiza madhehebu yote ya dini kuendelea kuhubiri amani, mshikamano na utulivu hasa katika kipindi cha kuelekea katika Uchaguzi Mkuu. “Amani na utulivu ni moja ya Tunu katika nchi yetu” Alisisitiza Mheshimiwa Majaliwa.
Akizungumza kuhusu tuzo hizo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa yanatoa nafasi ya kujenga maadili bora ikiwemo uaminifu, umakini, na kujitolea. “Washiriki wanajifunza umoja, upendo na mshikamano na wengine kwa ufanisi.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa mashindano hayo yanahamasisha jamii ya Kiislamu duniani kote kuwa na utamaduni wa kujisomea na kuhifadhi Qur’aan Tukufu. “Hii inachangia kuendeleza utamaduni wa kuheshimu dini, kudumisha maadili mema, amani na kuimarisha imani katika jamii”.
“Mashindano haya yanawawezesha vijana na watoto kuonesha uwezo wao katika usomaji na uhifadhi wa Qur’aan Tukufu. Hii ni fursa muhimu kwao kukuza kipaji, kujivunia mafanikio yao, na pia kujenga nidhamu na uwajibikaji. ”
Ameongeza kuwa Serikali inaamini mashindano hayo yatasaidia kuleta maendeleo ya kiroho kwa vijana na kuhamasisha jamii kwa ujumla. “Serikali itaendelea kushirikiana na jumuiya na taasisi mbalimbali katika kukuza na kuhamasisha shughuli za kidini”.
Naye, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zuber Bin Ally amewataka waumini wa kiislam nchini kudumisha amani na kuepuka kujiingiza katika viashiria vyovyote vinavyoweza kusababisha mmomonyoko wa maadili. “Nchi yetu kote duniani inasifika kwa kutunza amani tuliyonayo, tuendelee na utamaduni huu. ”
Mashindano hayo yameandaliwa na Jumuiya ya kuhifadhisha Qur’an Tanzania ambayo yanalenga kutoa fursa kwa Waislamu kutoka sehemu mbalimbali duniani kuonesha uwezo wao katika kuhifadhi na kusoma Qur’an Tukufu kwa usahihi na umakini mkubwa.
Washindi wa tuzo hiyo kwa washiriki wenye umri zaidi ya miaka ishirini ni Mohamed Amin Hassan mshindi wa kwanza kutoka nchini Marekani, Ismail Ally mshindi wa pili kutoka Kutoka nchini Libya na Malik AbdulAzizi mshindi wa tatu kutoka nchini Saudi Arabia.
Kundi jingine ni Washindi wa tuzo hiyo kwa washiriki wenye umri chini ya miaka ishirini ni Mohamed Yacine mshindi wa kwanza kutoka nchini Algeria, Yusuf Yasin mshindi wa pili kutoka nchini Uganda na Zayd El Bakkal mshindi wa tatu Kutoka nchini Moroco.