
Wananchi wanaotumia barabara ya Kibondo-Nduta iliyopo kijiji cha Biturana kata ya Nengo, Halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma wamesema ujenzi wa barabara hiyo utafungua fursa mbalimbali huku wakiishukuru serikali kupitia TARURA kwa kutatua changamoto ya ubovu wa barabara hiyo.
Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo barabara hiyo inapita wamesema kuwa ujenzi wa barabara utarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
Mkazi wa kijiji cha Biturana, Bw. Dickson Rugendanye ameeleza barabara hiyo imeweza kuwasaidia wajawazito waliokuwa wanapata changamoto kwenda kujifungua kufika hospitali kwa urahisi, pia imewasaidia wakulima kufika mashambani na kusafirisha mizigo na mazao yao bila shida yoyote.
Naye, Bw. Joshua Isaka mkazi wa kijiji cha Nyampengire mtoni ameishukuru serikali sasa wanasafirisha mizigo bila shida pia wanafunzi wanafika shuleni bila shida.
Akizungumzia barabara hiyo, msimamizi wa mradi kutoka TARURA wilaya ya Kibondo, Mhandisi Sambi Ngusa amesema mradi wa RISE sehemu ya uondoaji vikwazo katika barabara ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 85 umejumuisha ujenzi wa barabara ya Kibondo-Nduta Km 3.3 kiwango cha changarawe, makalavati manne (4), mifereji ya maji ya mvua Km 1.28 na vivuko 20 vya waenda kwa miguu.
Amesema kuwa, wanategemea mkandarasi kumaliza kazi hivi punde kwasababu anaendelea na kazi na kwamba wanaendelea kuboresha miundombinu ili wananchi waweze kusafiri bila shida, hivyo wanaishukuru serikali kwa kuongezea bajeti ya TARURA wilaya ya Kibondo kwa ajili ya kuboresha miundombinu.