Home LOCAL TANZANIA , UJERUMANI KUSHIRIKIANA UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

TANZANIA , UJERUMANI KUSHIRIKIANA UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!
Na WAF – DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za Afya bila kipingamizi chochote.
Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, leo Februari 18, 2025, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, katika kikao cha pamoja na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kilichofanyika ofisi za Wizara, jijini Dodoma.
Dkt. Magembe amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kutekeleza vipaumbele mbalimbali vya sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi wote wanakuwa na bima ya afya na uhakika wa matibabu.
“Kuimarisha mifumo ya taarifa ni hatua muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unafanikiwa. Mifumo thabiti ya taarifa itawezesha ukusanyaji, uchakataji, na usambazaji wa takwimu sahihi za afya, hivyo kusaidia kufanya maamuzi bora, kufuatilia maendeleo, na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi,” amesema Dkt. Magembe.
Aidha, Dkt. Magembe ameeleza kuwa wananchi wanapaswa kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya na faida wanazoweza kupata kupitia mfuko huu.
Aidha. Dkt Magembe ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha utekelezaji wa mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote. 
“Kupitia ushirikiano huu, Tanzania itaweza kutoa huduma bora za afya kwa wananchi na kuwa na mfuko wa bima ya afya jumuishi unaowanufaisha wote, bila kujali hali zao za kiuchumi,” amesema Dkt. Magembe
Kwa upande wake, Mkuu wa Programu wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) Bw. Kai Straehler-Pohl amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Ujerumani ni kuhakikisha Serikali ya Tanzania inatekeleza mpango huu kwa ufanisi, ili wananchi wote wapate huduma za afya kupitia mfuko wa bima ya afya.
“Ushirikiano huu utakuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha hatua zilizosalia zinatekelezwa kwa mafanikio, jambo ambalo litaisaidia nchi kufanikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa urahisi kwa wananchi wote,” amesema Bw. Kai.