Home INTERNATIONAL TANZANIA NA ALGERIA KUKUZA DIPLOMASIA YA UCHUMI

TANZANIA NA ALGERIA KUKUZA DIPLOMASIA YA UCHUMI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kilichofanyika tarehe 12 na 13 Februari, 2025 Addis Ababa, Ethiopia.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Serikali za Tanzania na Algeria zimekubaliana kukuza diplomasia ya uchumi kwa kutumia fursa muhimu za kiuchumi zinazopatikana katika nchi hizo mbili ili kujenga ustawi wa watu wake.

Hayo yamejiri wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kilichofanyika tarehe 12 na 13 Februari, 2025 Addis Ababa, Ethiopia.

Viongozi hao wamejadili juu ya umuhimu wa maandalizi ya Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria ambapo mara ya mwisho mkutano huo ulifanyika mwaka 2023 jijini Algiers, Algeria. Mkutano ujao ulikubaliwa kufanyika mwaka 2025 nchini Tanzania hivyo, wamekubaliana kuitisha mkutano mwingine mapema ili kuendana na makubaliano ya kuanzishwa kwa tume hiyo yanaoelekeza kuitishwa kwa mkutano huo  kila baada ya miaka miwili ili kuruhusu ufuatiliaji wa utekelezaji katika maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa.

Pia wamejadili kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu ambapo, Mhe. Attaf ameahidi kuwa Algeria itaendelea kutoa fursa za ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa lengo la kujenga uwezo na uzoefu katika masuala mbalimbali ya kitaaluma na kitaalamu.

Vilevile wamesisitiza umuhimu wa kukuza ushirikiano katika sekta ya biashara, nishati na kwenye masuala ya ulinzi, usalama. Pia, uwekezaji katika uzalishaji wa mbolea itakayotosheleza mahitaji halisi ya wakulima nchini Tanzania na kuwezesha kuyafikia malengo ya Mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ya kuongeza ajira kwa vijana na kufanya kilimo biashara.

Ushirikiano katika majukwaa ya kikanda na kimataifa ni miongoni mwa masuala yaliyopewa msisitizo ili kuhakikisha nchi hizo mbili  zinasimama imara katika kuunga mkono masuala ya kimkakati na yenye maslahi kwa pande zote katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.