Home LOCAL SHILINGI BILIONI 3 KUBORESHA MIUNDOMBINU YA HOSPITALI YA RUFAA KANDA YA KUSINI

SHILINGI BILIONI 3 KUBORESHA MIUNDOMBINU YA HOSPITALI YA RUFAA KANDA YA KUSINI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kuanza awamu ya pili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini – Mtwara, ambapo kazi zinatarajiwa kuanza ifikapo Aprili 2025.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Mkoa wa Mtwara Mhe. Abdallah Dadi Chikota, amesema fedha hizo zitatumika kujenga jengo la mama na mtoto, nyumba za watumishi, kichomea taka, na jengo la kufulia.

“Usanifu wa michoro umeshakamilika na tayari taratibu za kumpata mkandarasi zimeanza, huku zabuni ikiwa imeshatangazwa, na ndani ya wiki mbili tutakuwa tumekamilisha hatua hii,” amesema Dkt. Mollel.

Aidha, Dkt. Mollel, amethibitisha kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha ujenzi huo unaanza kama ilivyopangwa, ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa mikoa ya kusini.

Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini inatoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, na maeneo jirani, uboreshaji wa miundombinu ya Hospitali hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuboresha huduma za afya nchini.