Na Josephine Majura, WF – Dodoma
Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!Serikali imesema kuwa asilimia 20 ya mapato ya kodi zitarejeshwa katika halmashauri husika baada ya Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuhusu kuboresha usimamizi na ukusanyaji wa kodi hiyo utakapo kamilika.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe. Hassan Seleman Mtenga wakati ambao Serikali itarejesha makusanyo ya Kodi ya Ardhi ya asilimia 20 kwa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Mhe. Dkt. Nchemba alisema Serikali kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2023/24 ilifanya marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 kwa kuzitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuingia Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) katika usimamizi na ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi na kuweka utaratibu wa urejeshaji wa asilimia 20 ya mapato kwa halmashauri ili kuziwezesha katika ufuatiliaji na ukusanyaji wa mapato hayo.
“Serikali iliweka utaratibu huo ikiwa na lengo la kuhakikisha kuwa kuna tija katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na pango la ardhi inaongezeka na kuondoa kero zilizokuwa zinawakabili walipa kodi kwenye maeneo husika”, alibanisha Dkt. Nchemba.
Alilihakikishia Bunge kuwa Mkataba huo utakapokamilika na kuwasilishwa Wizara ya Fedha, fedha hizo zitarejeshwa kama utaratibu unavyotaka.