Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo ameeleza ndoto yake ya kuurejesha Mkoa wa Tanga hadhi yake ya kuwa mkoa wa viwanda, akilenga kufanya hivyo kwa kuweka sera thabiti na kujenga mazingira ya kuvutia uwezekaji.
Rais Dkt. Samia ameeleza hayo leo mbele ya maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mkwakwani.
Vilevile, Rais Dkt. Samia ameeleza dhamira yake ya kuhakikisha Mkoa wa Tanga unakuwa pia mkoa wa utalii na kuwa unanufaika zaidi na fursa zitokanazo na fukwe, historia na tamaduni mbalimbali ndani ya mkoa huo.
Akizungumzia ziara yake ya wiki moja katika Mkoa wa Tanga, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa wananchi kutumia ipasavyo fursa za maendeleo zitokanazo na miradi mbalimbali na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ndani ya Mkoa wa Tanga.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha vijana wanapata ujuzi na stadi stahiki ikiwemo kupitia shule, vyuo vya VETA viliyojengwa katika kila wilaya, Chuo cha Mafunzo ya Amali cha Mkoa na kampasi ya Chuo Kikuu Mzumbe kinachotarajiwa kujengwa katika Wilaya ya Mkinga, ili waweze kunufaika zaidi na miradi mbalimbali inayofanyika katika mkoa huo.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amezungumzia changamoto ya viwanda na mashamba yaliyobinafsishwa na Serikali kutoendelezwa kinyume na makubaliano ya ubinafsishaji, hali inayowanyima wananchi fursa mbalimbali ikiwemo za uzalishaji, ajira na masoko ya mazao yao.
Hivyo, Rais Dkt. Samia amesema Serikali itapitia mikataba ya ubinafsishaji ya viwanda na mashamba ambayo hayajaendelezwa na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria kwa lengo la kuhakikisha kuwa viwanda na mashamba husika yanawanufaisha wananchi.
Kesho tarehe mosi Februari 2025, Rais Dkt. Samia anatarajia kuhitimisha ziara yake ya wiki moja mkoani wa Tanga, ambapo pamoja na mambo mengine atafanya ziara kwenye Bandari ya Tanga iliyofanyiwa maboresho makubwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha utendaji na uwezo wa bandari hiyo.
Sharifa B. Nyanga
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu