Home BUSINESS NFRA KUUZA TANI MILIONI MOJA YA MAZAO 2025/2026

NFRA KUUZA TANI MILIONI MOJA YA MAZAO 2025/2026

Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam
Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula nchini (NFRA) unatarajia  kuuza takribani tani milioni moja za chakula  kwa mwaka wa fedha wa 2025/ 2026 kupitia masoko yaliyopo kwenye nchi tofauti zenye mikataba ya kuuziana mazao na shirika hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa NFRA, Dkt Andrew Komba amesema kuwa moja ya majukumu ya shirika hilo ni kuhakikisha usalama wa kutosha wa chakula hapa nchini  na kuuza chakula cha ziada kwa nchi zenye uhitaji kama moja ya sehemu ya kuwawezesha wakulima kiuchumi na nchi kujipatia fedha za kigeni.
 Amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne,  NFRA imeweza kuuza takribani tani 600,00 za mahindi , mtama  mpunga, dengu na mbaazi kwenye masoko ya India pamoja na China.
Amesema mafanikio haya na mipango iliyopo yanatokana na uwezeshwaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kulijengea uwezo shirika hilo.
“Miaka minne iliyopita, NFRA ilikuwa na uwezo wa kuuza kati ya tani 50,000-60,000 tu za nafaka,”
 “Lakini baada ya kujengewa uwezo, ufanisi uliongezeka ambapo miaka miwili iliyopita tuliweza kuuza tani 600,000 baada ya wananchi kuanza kufanya kilimo chenye tija na kuzalisha mazao yenye ubora  kulingana na maelekezo ya wataalamu hususani katika kilimo cha Mahindi na Mchele ,” amesema.
Amesema kuwa jitihadi za NFRA katika kutafuta masoko ya nafaka mwaka 2024 ilifanikiwa kupata mkataba wa kuuza tani 650,000 kwenda Zambia na mpaka sasa nusu ya tani hizo tayari zimeshapelekwa katika nchi hiyo na mkataba  huu unatarajiwa kufikia ukomo ifikapo mwezi Mei mwaka huu.
 Pia NFRA ilifanikiwa kuuza tani nyingine 500,000 katika soko la Jamhuri ya Congo (DRC) na kuuza tani nyingine 35,000 kwenye Shirika la Program ya Chakula duniani (WFP) ambapo kupitia mikataba hii, NFRA kwa ujumla imefanikiwa kuuza jumla ya tani 1,185,000 kutoka katika mashirika hayo.
Mbali na masoko yaliyopo katika nchi za Zambia na Congo (DRC), Malawi na  Zimbabwe, Dkt Komba pia amesema kuwa nchi ya Msumbiji pia wametuma maombi yao ya kutaka kununua mazao katika shirika hilo.
Ameongeza kuwa tayari nchi ya Malawi imeingia mkataba na NFRA wa kuuziwa  takribani tani 50,000 za chakula na kati ya tani hizo, wameshasaini makubaliano ya kuchukua tani 20,000 za kuanzia.
“Haya yote yanafanyika ni juhudi na jitihada za Serikali ya Rais Samia  ambapo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, NFRA imefanikiwa kupanua ukubwa wa masoko yake katika nchi za kimataifa na kupelekea kuongeza tija na thamani ya mazao na kilimo chetu nchini” Alisema Dkt Komba na kuongeza;
 “Tumekuwa tukiongeza nguvu ya mauzo yaliyotokana na chakula cha ziada ili kukidhi uhitaji wa soko la kimataifa ili kuwafaidisha wakulima wengi kutokana na chakula tunachoki nunua kutoka kwao kwa ajili ya akiba ya chakula hapa nchini na ziada kuuza nje ya nchi,” amesema.
 “ Ni jukumu kubwa la NFRA kutafuta masoko ya nje ya nchi kwa chakula cha ziada kinachozalishwa hapa nchini, ili kuongeza tija katika kilimo kwa wazalishaji wote katika mnyorororo wa thamani,” amesema.
Katika kuhakikisha usalama wa chakula unakuwepo  hapa nchini na kuzalisha chakula cha ziada kwa ajili ya kuuza nje ya nchi, Dkt Komba amesema mamlaka hiyo imekuwa ikiwahimiza wananchi kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija ili kuhakikisha mazao yanakuwa yenye ubora unaohitajika katika masoko ya kimataifa kwani ndio njia pekee itakayo iwezesha NFRA kupata masoko ya uhakika.
 Mwisho.