Home BUSINESS NFRA KUKABIRIANA NA UPUNGUFU WA SUKARI

NFRA KUKABIRIANA NA UPUNGUFU WA SUKARI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na Mwandishi Wetu

WAKALA wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA) umesema umejipanga vizuri kukabiliana na upungufu wa sukari hapa nchini endapo kutajitokeza upungufu wa bidhaa hiyo kwani serikali imeshatoa kibali kwa wakala kuagiza na kusambaza sukari.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam , Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dk Andrew Komba amesema NFRA imepewa jukumu la ununuzi wa sukari nje kwa ajili ya kutosheleza soko la ndani pale uhaba utakapojitokeza kwa lengo la kuwa na akiba ya kutosha kwa kipindi cha miezi miwili kama sheria ya sukari inavyosema.

Sheria ya sukari inasema kwamba, “endapo NFRA itagundua kuna uhaba wa sukari itatoa sukari yake iliyoihifadhi na kuiingiza sokoni,”

“Lakini pia endapo mojawapo ya kiwanda au viwanda vyote vikashindwa kuzalisha, basi NFRA itatoa sukari yake iliyoiagiza na kuiingiza sokoni” amesisitiza Dk Komba.

Dk Komba amebainisha kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria hiyo na kuipa nguvu taasisi hiyo kuwa na sukari ya kutosha muda wote na siyo kusubiri mpaka pale kunapokuwa na uhaba wa bidhaa hiyo muhimu.

“Malengo ya Serikali ya Rais Samia Sukuhu Hassan ni kuona Watanzaia wanapata mahitaji muhimu na kuhakikisha uwepo kwa akiba ya chakula cha kutosha ikiwemo sukari kwa usalama wa nchi,”

“ Na ndiyo maana baada ya kujengewa uwezo wa kutosha na Serikali, NFRA imeweza kuwa na akiba ya kutosha ya chakula ikiwemo sukari katika kukabiliana na upungufu wowote unaoweza kujitokeza,” amesema.

Dk Komba amesema kwa upande wa nafaka, wakala umeweza kuhifadhi akiba ya kutosha ya chakula ziada kuuza nje ya nchi.

“Lakini pia kwa upande wa sukari, tunahakikisha kuwa ipo ya kutosha ili kukabiliana na upungufu hasa pale viwanda vinaposhindwa kuzalisha au kuagiza kutoka nje ili kuhakikisha nchi inakuwa na bidhaa hiyo muhimu muda wote ili kukabiliana na upungufu unaoweza kujitokeza,” amesema Dk Komba.

Amesema kuwa Serikali imeipa taasisi yake mamlaka ya ununuzi na kuhifadhi sukari kutokana na changamoto ya uhaba wa bidhaa hiyo kujitokeza mara kwa mara miaka iliyopita na kuleta usumbufu kwa wananchi.

“Tumelipokea jukumu hili kwa mikono miwili na utekelezaji wake unakwenda vizuri,” amesema Dk Komba.

Mwaka jana, wakati Rais Dk Samia Suluhu Hassan alipokuwa ziarani mkoani Morogoro, alifungua kiwanda cha sukari cha Mkulanzi ambacho kinamilikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza, ambapo alisema kuwa lengo la uwepo wa kiwanda hicho ni kuongeza kiasi cha uzalishaji sukari hapa nchini.

Wakati wa ziara hiyo, Rais Samia alisema kuwa kati ya mwezi Machi mpaka Mei (mwaka Jana), kulikuwa na upungufu wa sukari, hivyo serikali ikaagiza sukari nje ya kutosha na kupelekea bei yake kushuka ili kuwasadiai wananchi kuipata bidhaa hiyo kwa bei nafuu.

pamoja na hayo, Dkt Komba alisema serikali kupitia Waziri wa Kilimo Bw. Hussein Bashe ilisema kuwa katika kukabiliana na upungufu wa sukari uliokuwa unajitokeza, serikali ipo tayari kufanya kazi na taasisi binafsi kwa ajili ya kuhakikisha sukari inapatikana kw uhakika nchini na kuwataka wafanyabiashara wawe waaminifu na wasipandishe bei ya sukari.

Viwanda vinavyozalisha sukari hapa nchini ni pamoja na kiwanda cha Kilombero, Mtibwa, Bagamoyo, TPC Limited na kiwanda cha Serikali cha Mkulazi .

MWISHO.