Home LOCAL MSIGWA: WANAHABARI TUONGEZE UMAKINI KUEPUSHA TAHARUKI

MSIGWA: WANAHABARI TUONGEZE UMAKINI KUEPUSHA TAHARUKI

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa akizungumza na wahariri wa habari katika kikao chake kilichofanyika leo taehe 18 Februari 2025, Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akizungumza katika kikao hicho Jijini Dar es Salaam.
DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amewakumbusha wanahabari kuwa makini kwenye uandishi wa habari ili kuepusha taharuki kwenye jamii. 
Akizungumza na wahariri wa habari katika kikao chake kilichofanyika leo taehe 18 Februari 2025, Jijini Dar es Salaam Msigwa alisema, peni za waandishi wa habari ni kama ‘risasi.’inayoweza kuleta madhara kwa jamii.
Msigwa alitoa kauli hiyo baada ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile katika ufunguzi wa kikao hicho kueleza tahadhari inayoweza kushusha thamani ya chombo cha habari pale stori moja pekee inapokuwa na makosa.
“Kunapokuwa na kosa kwenye stori moja katika gazeti lenye stori 100 halafu ukasema gazeti ni feki, hii sio sawaswa, tunaamini maelezo kuhusu haya tutayapata,” alisema.
Msigwa alisema, pale makosa yanapotokea huulizwa kwa kuwa ndiye msimamizi wa vyombo vya habari nchini, nakwamba kuna taarifa ambazo zikitolewa, taharuki yake huwa kubwa.
“Kuna chombo kimoja kiliandika kuhusu tamko la Rais wa Marekani kuhusu dawa za ARVs (za kupunguza makali ya Virusi vya UKIMWI).
“Tukalazimika kuweka taarifa hii haraka, maana ingeweza kusababisha taharuki, tukasema tuna akiba ya miezi sita ili kuweka mambo sawa,” alisema.
Alisema, taarifa kama hii inaweza kusababisha hofu kwa watumiaji wa dawa hizo kwamba, itakuwaje ama ndio watakufa.
“Tukaamua kufanya hivyo tulivyofanya hata kama kuna makosa kidogo lakini ilibidi tufanye haraka ili kuepuka taharuki,” alisema.
Kwenye kikao hicho, Msigwa alifikisha salamu za Rais Samia Suluhu Hassan kwa wahariri na kuahidi kuendelea kushirikiana na wanahabari kukuza sekta hiyo.
“Kabla ya kuja hapa, nilizungumza na Rais kumueleza kwamba ninakwenda kuzungumza na wahariri, aliniambia wasalimie na ataendelea na juhudi za kuhakikisha sekta inaimarika zaidi.
“Niwahakikishie serikali haina dhamira yoyote ya kubana vyombo vya habari nchini, mpango huo haupo na hautakuwepo. Tunataka Tanzania iwe mfano wa Uhuru wa Vyombo vya Habaari,” alisema.